Mkoa wa Dodoma unashuhudia maendeleo makubwa na ya kasi kwa kipindi kifupi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo Mkoa umeamua kuyaweka wazi kupitia maadhimisho ya siku ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni maalum kwa kumpongeza na kumshukuru, yaliyopewa jina la ‘Dodoma Samia day’ yaliyofanyika Juni 03, 2025 katika kata zote 209 zinazopatikana katika Halmashauri 8 za Mkoa wa Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameshiriki Maaadhimisho hayo kwenye Kata ya Makole Jijini Dodoma ambapo makundi mbalimbali yalihudhuria kwa lengo la kuyasema mazuri hayo.
“Yupo mtu ambaye amefanya vitu vingi ambavyo katika historia ya Nchi yetu tangu Uhuru hatujawahi kushuhudia maendeleo ya muda mfupi kwa kasi kubwa kwa Mkoa wa Dodoma kama tulivyoshuhudia katika kipindi hiki. Tumesikia wakati wote watu wakisema, lazima vitu visemwe, tusipovisema sisi, wengine watasema kinyume chake.”
Amesema RC Senyamule Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesema katika Wilaya yake amepitia taarifa za miradi kwenye kila Kata jinsi ambavyo zimeguswa, ikiwemo miradi mikubwa ngazi ya Wilaya, miradi ya kimkakati na miradi ya wadau na kujiridhisha kwamba wametumia fedha zaidi ya shilingi Trilioni 1 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa Wilaya ya Dodoma pekee. Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Makole Mhe. Omary H. Omary amesema katika kipindi cha miaka mitano, Kata yake imepokea miradi mingi ikiwemo ujenzi wa Barabara za lami, madarasa ya muundo wa ghorofa katika shule ya msingi Makole, malipo ya fidia kiasi cha milioni 900 kwa wananchi waliokua wanasumbuliwa katika eneo la ‘D Center’ pamoja na ujenzi uliokamilika wa ofisi ya Machinga Mkoa. Mmoja kati ya mashuhuda wa mambo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha ‘Wanawake na Samia’ Mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Madidi, ameshuhudia mafanikio ya Serikali kwenye Kata ya Makole kwa upande wa nishati safi ya kupikia ya mkaa mbadala ambayo wao kama kikundi ni mawakala wa kuuza na kusambaza nishati safi.