
RC Senyamule Aviomba Vyombo vya Habari Kuhamasisha Upigaji Kura
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, ameviomba vyombo vya habari Nchini kutumia siku nne zilizobaki kuhamasisha wananchi kujitokeza Oktoba 29, 2025 kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. Ombi hilo linakuja wakati zikiwa zibaki siku nne kwa Watanzania, kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakao waongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Mhe.

Senyamule,amesema hayo Jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhamasishaji wa makundi mbalimbali ya wananchi kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi Mkuu, 2025. Amesema , vyombo vya habari Nchini vinao uwezo mkubwa wa kuhamasisha Wananchi kujitokeza kupiga kura kutokana na imani kubwa waliyonayo kwa tasnia hiyo. “Kama kwa siku hizi chache mtatumia ipasavyo vyombo vyenu vya habari kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura, basi ninaamini kuwa watu wengi watajitokeza kushiriki zoezi hili muhimu la kikatiba na kuiondoa Dodoma kwenye idadi ya mikoa itakayofanya vibaya,”amesema Mhe. Senyamule Aidha,amesema Mkoa umeweka mikakati ya kuhamasisha

Wananchi kushiriki Uchaguzi kwa kukutana na makundi mbalimbali ili kuyapa elimu juu ya umuhimu wa kupiga kura. Kadhalika, Mhe. Senyamule amesema takwimu zinaonesha mkoa wa Dodoma haukufanya vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu 2020, hivyo mwaka huu hawataki hali hiyo ijirudie. “Mwaka 2020 Mkoa huu haukufanya vizuri kwani kati ya asilimia 100 ya watu waliojiandikisha kupiga kura ni asilimia 45 tu ndiyo walipiga kura, hivyo asilimia 55 hawakujitokeza kupiga kura.

“Lakini pia katika jiji la Dodoma hali ilikuwa mbaya zaidi kwani kati ya asilimia 100 ya waliojiandikisha waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 20 hivyo asilimia 80 wote hawakupiga kura hivyo tunatamani hali hii isijirudie tena mwaka huu,”Amesisitiza Mhe Senyamule. Vile vile,ametaja baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikisababisha watu kutojitokezi kupiga kura ni pamoja na jamii kukosa uelewa wa umuhimu wa kushiriki mchakato huo wa kikatiba.






