MAPOKEO YA TAMADUNI MPYA YASIWE KIKWAZO CHA KUIMARISHA NDOA KWENYE FAMILIA..SOMA HAPA ZAIDI

Special Correspondent7 years ago8 Views

Image may contain: 1 person, smiling, closeup
Na Debora Charles✍🏾
Kiungo pekee ambacho huchochea misingi ya familia bora katika maisha ya watu wengi ni ndoa. Ndoa huzaliwa kutokana na hisia za upendo baina ya watu wawili walioaminiana na kuamua kuungana, kuishi pamoja mpaka kifo kwa lengo la kutengeneza familia bora ya watoto wenye afya njema. Hata hivyo mabadiliko ya mazingira, masuala ya ujana na mapokeo ya tamaduni mpya yamekuwa yakiathiri ndoa nyingi na hata kupelekea ongezeko kubwa la kuvunjika kwa ndoa hizo jambo ambalo linaashiria ujio wa athari nyingi kwa vizazi vijavyo.
Utafiti wa Ufatiliaji wa Kaya Tanzania (National Panel Survey) uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2014/15 na kuchapishwa mwaka jana 2017 ulibaini kuwa kasi ya wanandoa nchini kupeana talaka imeongezeka mara mbili ndani ya miaka 6 hivi karibuni, jambo ambalo linatishia mustakabari wa taasisi hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.
Utafiti huo ulionyesha, kiwango cha talaka kilikuwa kimeongezeka kutoka asilimia 1.1 mwaka 2008/9 hadi asilimia 2.1mwaka 2014/15. Hii inamaanisha kwamba kwa sasa kila watu 100 wenye umri wa kuoa au kuolewa waliopo nchini 2 wametalakiwa kutoka 1 kwa mwaka 2008/2009. Mbali na talaka, kuna wanandoa takribani 4 kwa kila 100 ambao wametengana jambo linaloashiria huenda nao wakatalakiana siku zijazo iwapo hawatapata suluhu ya kudumu ya tofauti zao.
Matokeo ya utafiti huo yanakwenda sanjari na yale ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 yaliyobainisha kuwa Watu 715,447 walikuwa wametalakiwa mwaka 2012 (sawa na watu 3 kwa kila 100) wenye umri wa kuoa au kuolewa na wanandoa 232,415 walikuwa wametengana mwaka 2012 (ambayo ni takribani watu 4 katika 100)
Pamoja na umaskini na mtazamo wa tamaduni baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa kuolewa kuchochea NDOA ZA UTOTONI, hali ya kutengana au KUTALAKIANA baina ya wanandoa itashika nafasi kubwa ya kuongezeka kwa wimbi la ndoa za utotoni kwa vizazi vijavyo endapo kama haitapata suluhu ya kudumu.
Ripoti ya Utafiti wa visababishi na madhara ya ndoa za utotoni Tanzania iliyofanywa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Shirika la kutetea haki za watoto (Plan International), Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) pamoja na Shirika la Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA) ilibaini kuwa watoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 (kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha Dunia ambacho ni watoto 34 katika kila watoto 100) na watoto 27 wa kitanzania wanapata mimba kabla ya umri huo.
Hata hivyo MAENDELEO YA ELIMU yamechochea fikra za vijana wengi kuanza kujikita katika masuala ya ndoa wakiwa tayari wameweza kujisimamia katika nyanja mbalimbali za maisha ikiwemo uchumi. Jambo hili kwa kiasi kikubwa limechochea uhuru uliopitiliza katika kuchagua wenzi wa maisha yao na hata kupelekea wengi kupunguza THAMANI YA VIGEZO VYA MSINGI na vya kudumu na badala yake kuvutiwa na vigezo vya muda mfupi visivyoendana na uhalisi wa maisha ya ndoa.
Aidha Maendeleo ya elimu yamechochea kuondokana na njia rafiki ya kuwakutanisha wenzi hawa jambo linalopelekea wachumba wengi kukutana nje ya MAENEO YA MACHIMBUKO yao na hatimaye kufifisha nguvu ya kufahamiana kitabia na kihistoria baina ya wenzi hao.
Ni wazi kuwa mabadiliko ya tamaduni zetu na mifumo mipya ya maisha imeathiri mifumo mingi ya ndoa iliyokuwa ikitumika zamani. Ili kuimarisha mahusiano yetu ni lazima wachumba/wanandoa wakubali mabadiliko ya ulimwengu wa sasa. Ni lazima busara ziwaongoze kuondokana na mifumo gandamizi inayoumiza upande mmoja. 
Image may contain: 1 person, standing and outdoor
Kama ilivyo katika kazi au biashara, uchumba/ndoa nayo inahitaji UWEKEZAJI MKUBWA katika kuijenga na kuiimarisha. Unahitaji kuruhusu haja ya kutenga muda mwingi na mwenzi wako katika kushiriki naye matukio na nyakati mbalimbali, unahitaji kuwekeza katika kujisomea vitabu vya mahusiano, kusikiliza semina na mafundisho ya wataalamu wabobezi. Unahitaji kuwekeza akili nyingi katika kubuni njia rafiki za kuimarisha upendo hata katikati ya wimbi la misuguano.
Ni lazima tuamini, TUKIRI na tukubali KUSAMEHE wakati wowote ambapo wenzi wetu watatukosea. Ni ukweli usiopingika kuwa binadamu yeyote si malaika hivyo kukosea ni jambo la lazima, kukiri msamaha kabla hujakosewa kunachochea amani na ustahimilivu pindi unapojeruhiwa. Kushindwa kusamehe ni kukaribisha uchungu, chuki, mashindano na hatimaye mafarakano baina yenu.
Ni lazima nguvu ya ushawishi itokane na msukumo unaokuaminisha USAHIHI WA WAKATI NA MTU unaeanza naye kuhusiana. Tuepuke kutarajia mambo yanayotufurahisha kwa muda mfupi badala yake tusukumwe na kiu ya kuanza kutafuta pamoja vitu vyote vinavyotuvutia.
Lazima tujenge utaratibu wa KUWAFATILIA wenzi wetu katika maeneo yao ya makuzi/historia ili kujua machimbuko, koo, afya (kufahamu magonjwa ya kurithi nk) na hata tamaduni wanazojihusisha nazo. Hii itasaidia kuwakubali jinsi walivyo na kuwa tayari kustahimili vishindo vya hali na tabia zao katika kipindi cha maisha yote ya ndoa.
Maisha halisi huleta tathmini halisi katika kumtambua mwenzi uliyenaye. Lazima TUUISHI UHALISIA wa maisha yetu pindi tunapoanza mahusiano ili kuziruhusu fikra zifahamu tabia na mienendo halisi baina yetu hususani tunapokutana katika mazingira ya tofauti na machimbuko yetu.
Ni lazima kila wakati, tujenge utamaduni wa kukubali KUJIFUNZA ili kubuni namna bora ya kuboresha mahusiano yetu na wenzi wetu. Ni elimu ya mahusiano pekee ndiyo itatusaidia kujua tofauti kati ya mwanaume/mwanamke na mume/mke. Itatufumbua kujua njia zinazotumika katika kuimarisha ndoa kwa kuvumiliana, kusikilizana, kukubalina na kutulizana kwa hali yoyote ili kulinda mahusiano.
Lazima tukubali KUACHA matumizi ya MITANDAO YA KIJAMII yaliyopitiliza pindi tunapokuwa na wenzi wetu. Tukumbuke Kutenga muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii ni kuwatenga wenzi wetu na kuwafanya waamue kutoka nje ya mahusiano tuliyonayo.
Ipo haja ya KUKUBALI KUBADILIKA na kuzifanya tamaduni mpya zichochee ndoa imara kwenye jamii zetu…
Debora Charles ni Mwanadada Msomi na Mwananzuoni aliyejikita zaidi katika kuelimisha jamii kwa njia ya mafundisho na machapisho mbalimbali ya Siasa na Mahusiano akiigusa jamii kwa ujumla..
Umenipenda?
 SHARE NA WENGINE WAISOME
Join Us
  • Facebook38.5K
  • X Network32.1K
  • linkedin12.6k
  • youtube23.4k
  • Instagram18.9K
Mchanganyiko
Loading Next Post...
Follow
Sign In/Sign Up Search Trending
Popular Now
Loading

Signing-in 3 seconds...

Signing-up 3 seconds...