Ni
kweli kuachwa kunaumiza sana moyo. Kimsingi usiombe kukumbwa na maumivu
ya kuachwa. Lakini kama hilo limekwishatokea, kwa nini uendelee kuumia
na kumchukia aliyekuwa mpenzi wako?
Kitendo cha kukuacha wewe,
kinaweza kumtokea hata yeye na kujikuta akilia na kuhuzunika kama wewe.
Kama ndivyo basi mapenzi ndivyo yalivyo. Leo kwako, kesho kwake.
Hakuna
sababu ya kuchukiana na kuwekeana visasi kwa sababu kama tutafanya
hivyo, kwa dunia ya sasa iliyojaa uchepukaji, itakuwa dunia ya visasi
kila kukicha.
Ifahamike kwamba, mapenzi hayana fomula,
inawezekana mwenza wako akawa amerubuniwa na kuna siku atarejea kwako na
kutulia kama unavyotaka.
Siwatetei wenye tabia ya kuacha, wala
siyo tabia nzuri kubadilisha wapenzi, lakini pengine ni ujana ndiyo
unamsumbua au ni tabia asili ya mwenza wako, tabia ambayo haipaswi
kuigwa na ni hatari kiimani, kimaadili na hata kiafya.
Ninavyofahamu
mapenzi ni kitu cha ajabu sana, inawezekana mkawa mmeachana kwa muda
kwa maana ya kupumzishana au kuna mtu kaingilia kati penzi lenu au
mmeachana moja kwa moja.
Haijalishi ni aina ipi ya kuachana ila
ninachozungumzia ni kuachana au kuachwa na kujenga chuki, hakuna sababu
kwa namna mapenzi yalivyo kwa sababu utachukia wangapi? Hivi kwa mfano,
ukiachwa au kuachana na wapenzi watano na wote ukawachukia, si utakuwa
umetengeneza bomu la hatari katika maisha yako? Kwa sababu utakuwa
ukiwaona moyo wako unaumia na kuwaza mabaya juu yao.
Kama
mlikuwa mnajua mtakuja kugombana, hamkuwa na sababu ya kuanzisha
uhusiano wa kimapenzi na kama mlilazimishana, kupendana hakuna sababu ya
kuchukiana. Naamini hamkujua kama mtakuja kugombana ndiyo maana mliamua
kupendana na ‘kushea’ baadhi ya vitu vyenu.
Sidhani kama mliamua kuwa wapenzi ili mje kupeana stress (msongo), mgombane, mchukiane, muharibiane maisha na mambo mengine.
Kama
umeachwa kwa sababu za msingi, kubaliana na ukweli ili maisha yasonge
kuliko kuendelea kufikiria na kutengeneza chuki na uhasama na mtu
aliyekuacha au kuachana, haisaidii kitu, kama wewe unavyohisi kutendwa
na yeye huko alikokwenda anaweza kutendwa vilevile. Mapenzi ni mchezo
usiokuwa na bingwa.
Angalizo; kwa wale wenye tabia ya kuacha hovyo, haipendezi kwani kuna mambo mengi ambayo unaweza kuyatengeneza bila kujua.
Wanawake
huamini kwamba unapomuacha, huwa umemchezea kwa maana ya kutimiza haja
zako na unapopata mtu mwingine ‘unamshiti’ bila kujua kuwa uhusiano wa
mapenzi ni kama kitabu ambacho kinapaswa kifunuliwe kurasa zake.
Inawezekana anayekifunua, akafunua kurasa moja na kukutana na andiko
alilokusudia au kufunua kurasa zaidi na zaidi.Tukutane wiki ijayo katika
mada nyingine tamu na nzuri.