NAKUKARIBISHA katika Jumanne tuliyoiona kwa kudra za
Mwenyezi Mungu kwa kutupa pumzi na uhai wake bure.Leo tutazungumzia
kuhusu suala zima la kuwa makini katika kuwashauri wapenzi
waliofarakana.
Kama
unataka kuwashauri watu walio na malumbano katika uhusiano wa mapenzi
basi kwanza washauri kwa kuutenga ukweli na uongo bila kuegemea upande
mmoja. Pili kuwa makini kuuponda upande mmoja ambao haupo karibu yako
wakati ukimshauri mwenza wake.
Kama upande usiokuwepo ukija kusikia kuwa uliuponda unaweza kudhani
ulifanya hivyo kwa sababu una masilahi yako binafsi kwa mwenza wake au
inawezekana unamtaka mwenza wake na ulifanya hivyo ili kuzidi
kumnyong’onyesha yeye huku wewe ukijitengenezea mazingira ya ushindi kwa
kutumia ugomvi wao.
Kwa wapenzi unaowashauri, kuna mawili baada ya ushauri wako,
inawezekana ukawa umetibu tatizo lao na wao kujijenga vizuri katika
uhusiano au ushauri wako ukabomoa kabisa uhusiano wao.Kama utafanikiwa
kuujenga na kuuimarisha uhusiano wao kwa maneno yako ni jambo jema
ambalo siku zote wao watajivunia kama wapenzi, lakini pia hata wewe
itakuwa ni furaha maishani mwako kuona wapendanao au ndoa ya f’lani
ikiendelea kudumu kwa sababu ya ushauri wako.
Lakini
kama ushauri wako utasababisha kuvunja uhusiano au ndoa ya wawili wale
ni dhahiri, mmoja wapo atajenga chuki na wewe kwa kuamini kuwa
ulichangia kwa asilimia kubwa kuvunjika kwa uhusiano wao.
Linapokuja suala la kuwashauri wapenzi walio kwenye mgongano au
wameachana unapaswa umshauri kuwa makini sana la sivyo unaweza
kujiingiza kwenye mgogoro usio kuhusu.Simaanishi usiwashauri ila jaribu
kuwa makini usije ukaegemea upande mmoja, kama utashauri basi simama
kwenye ukweli bila kumtetea mtu wa jinsi yako kama amekosa, kama
utamtetea basi utakuwa haujawasaidia kitu zaidi ya kumpa kichwa
aliyekosea na kujiona yuko sawa.
Endapo aliyekosea akibaini kuwa ulikuwa unamkandamiza kwa kumtetea
mtu wa jinsi yako, atachukia na kuamini watu wa jinsi ile wote hawana
maana na kumfanya atengeneze fundo la chuki moyoni mwake.