
Mradi huo uliozinduliwa Agosti 22, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango, unalenga vijana kuingia kwenye kilimo cha kisasa chenye thamani na tija.
“Hili ni jambo la kimapinduzi la kubadilisha Taifa. Hapa Dodoma tumepewa hazina kubwa sana ya maji chini ya ardhi. Kupitia miradi hii ya Kilimo cha umwagiliaji, Dodoma hakuna tena njaa, zile salamu za njaa hazitakuwepo tena kwani chakula kitakua kingi na kingine tutauza” Amesema Mhe. Dkt Mpango.
Mradi huo uliopewa jina la Dkt Samia Suluhu Hassan, unaotekelezwa kwenye eneo la ekari 11,000 utahusisha vijana 420 kutoka mikoa mbalimbali nchini huku vijana 50 wakiwa ni wazawa wa eneo hilo. Mpaka sasa ujenzi wa Miundombinu ya umwagiliaji imefikia 35% ambayo inagharimu shilingi Bilioni 21.6
Mara baada ya uzinduzi huo, Makamu wa Rais alifanya Mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Mpwayungu katika Wilaya hiyo ambapo ametoa maelekezo mbalimbali ikiwemo wafugaji wa eneo la Mradi watengewe eneo la malisho ili kuzuia kuingiza Mifugo kwenye eneo hilo.
Aidha, ametoa maelekezo kadhaa kama kujengwa kwa kituo cha Afya katika eneo la Mradi, TANROADS waboreshe Barabara kutoka Mpunguzi mpaka kwenye eneo la Mradi yenye urefu wa KM 100 ili kupitia Mradi huo, Barabara hiyo itawezesha Utalii kwenye mbuga ya Ruaha.
Mhe. Dkt. Mpango, amehitimisha ziara ya kikazi ya siku nne katika Mkoa wa Dodoma kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye Wilaya Sita za Mkoa wa Dodoma kwa fedha kutoka Serikali kuu ikiwa na lengo la kuboresha huduma kwa wananchi. Miradi hiyo ni ile ya sekta za Elimu, afya, maji, kilimo, n.k
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu






