Na Mwandishi Wetu
WAKATI jana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitikisa Jiji la Dar kwa kuanza kampeni za uchaguzi mkuu, Oktoba 25, mwaka huu, nyuma ya pazia ya tukio la Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye kuhama chama hicho kwenda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumeibuka mambo kibao, Uwazi limebainishiwa.
Kitendo cha Sumaye kuhamia Ukawa kwenda kumkutanisha na ‘hasimu’ wake kisiasa kwa miaka mingi wakiwa ndani ya chama kimoja, Edward Lowassa kimeshangaza.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, yapo mambo kadhaa nyuma ya pazia ya Sumaye kuhamia Ukawa lakini alichokisema yeye wakati anakaribishwa kwenye umoja huo, Agosti 22, mwaka huu kule Kunduchi jijini Dar ilikuwa kama rasharasha tu.

Frederick Sumaye akihutubia wanachama wea Chadema.
ANAKUWA MGOMBEA MMBADALA
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani kutoka kwa mtu mmoja ndani ya Ukawa, Sumaye asingeweza kuhama CCM kama asingeahidiwa kitu.
“Unajua bwana, kwa siasa za sasa nchini, Sumaye asingetoa miguu yake kwenda Ukawa. Alikaa kwanza na akina Mbatia (James, mwenyekiti mwenza wa Ukawa) na kufanya naye mazungumzo ya kina.
“Kimsingi walimwambia atakuwa mgombea mbadala wa Ukawa. Na kama yeye mwenyewe ulimsikia akisema amekwenda Ukawa kumsaidia Lowassa. Sasa we unadhani kumsaidia Lowassa kivipi?” alihoji mtoa habari huyo bila kufafanua umbadala huo kwani mgombea mwenza wa Ukawa ni Juma Duni Haji (ndiye msaidizi).
Ukawa inaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (Cuf) na NLD.
MADARAKA MAKUBWA
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, pia katika mazungumzo yao yaliyochukua siku kadhaa jijini Arusha wiki iliyopita, ili ‘kumlainisha’ Sumaye kutua Ukawa, walimuahidi cheo kikubwa serikalini endapo Ukawa itashika dola baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
KIKWAZO KIPO HAPA
Kwa maana hiyo, cheo kikubwa kilichobaki ni uwaziri mkuu, kwani makamu wa rais tayari yupo Juma Duni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, waziri mkuu anatakiwa kutoka katika ubunge wa kuchaguliwa na si wa kuteuliwa. Sumaye hajagombea jimbo lolote. Awali alikuwa mbunge wa Jimbo la Hanang, Arusha kupitia CCM.
HASIRA ZA KUONEWA NA CCM
Pia ilisemwa kuwa, kitendo cha Sumaye kukatwa jina lake kwenye mchakato wa wagombea urais kupitia CCM mjini Dodoma Julai mwaka huu, ni chachu kubwa iliyomsukuma kiongozi huyo kwenda Ukawa hasa baada ya kutendewa tukio kama hilo, mwaka 2005.
“Ndiyo maana hata mwenyewe alisema anajiona ndani ya CCM yeye ni mchanga kwenye kokoto na mawe. Kwa hiyo ukiangalia sana ameamua kwenda Ukawa ili kuwaumiza CCM wajutie kumkata kwake,” kilisema chanzo.
NI KWELI HAWAJASALIMIANA KWA MIAKA 20?
Habari nyingine kutoka duru za kisiasa nchini zinadai kuwa, Sumaye na Lowassa hawajapeana salamu kwa miaka takriban ishirini kufuatia uhasama wa kisiasa na si vinginevyo.
Uhasama huo unatajwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na harakati za kisiasa ambapo mwaka 1995 katika vuguvugu la uchaguzi mkuu, Lowassa alikuwa kwenye mtandao ulioratibiwa kumwingiza madarakani Jakaya Kikwete (rais wa sasa) Sumaye hakuwa mwanamtandao.
“Tangu kipindi hicho hawakuwa katika uhusiano mzuri hasa baada ya Benjamin Mkapa kumbwaga Kikwete kwenye uteuzi na kumfanya Sumaye kuwa waziri mkuu wake.
“Utakumbuka pia mwaka 2012, Sumaye aliwahi kumtuhumu Lowassa kwamba aliinjinia kushindwa kwake kwenye Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha ambapo Mary Nagu aliibuka mshindi.
“Leo tunapoambiwa kuwa Sumaye amekwenda kumsaidia Lowassa ni kauli ya kutatanisha sana,” chanzo chetu kilimaliza kwa kumshangaa waziri mkuu huyo wa awamu ya tatu.
WALICHEKEANA JINO PEMBE
“Siku ile ya Sumaye kutambulishwa Ukawa, walikumbatiana na kuchekeana lakini kwa jino pembe. Pale kila mmoja alikuwa na lake moyoni. Wale kihistoria siyo marafiki hata kidogo. tena hawana umoja. Kama watakuwa wamoja basi labda kwa sababu wameunganishwa na Ukawa,” kilisema chanzo.
FAMILIA BADO HAIKUBALIANI NA SUMAYE?
Pamoja na uamuzi huo wa kumfuata Lowassa Ukawa habari kutoka ndani ya familia ya Sumaye zimedai kuwa kumekuwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa ndugu. Wapo wanamuunga mkono na wengine hawakubaliani naye.
“Wengine wanasema kuwa kwenda Ukawa ni kujichonganisha na serikali kwa imani kuwa hawatashika dola hivyo wangependa mzee wao abakie CCM inayotarajiwa kushinda ili nao wapate fursa za kiserikali kama alizopata yeye kiasi cha kupewa uwaziri mkuu.” Chanzo.
Chanzo kiliongeza kuwa wakati ndugu hao wakipingana na uamuzi huo, wapo wengine wamefurahi kwa sababu mbili. Moja ni kutafuta heshima ya ndugu yao ambaye amekuwa akidharauliwa na chama chake na pili ni imani kuwa, Ukawa watashinda urais kwa nguvu ya mchango wa ndugu yao.