Na Mwandishi Wetu, Nairobi
SUALA la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka ukanda wa mafuta wa Uganda kwenda Pwani ya Afrika Mashariki limechukua suala mpya katika uhusiano wa nchi tatu za Kenya, Uganda na Tanzania.
Taarifa zinaonesha kuwa mradi huo mkubwa unaolenga kuisaidia Uganda kusafirisha raslimali yake hiyo kwenda katika masoko ya dunia utagharamu dola za Marekani bilioni 4.5 (iwapo utajengwa Kaskazini mwa Kenya) na dola bilioni 4.0 pekee (iwapo utajengwa kupitia Tanzania) lakini kumeibuka majadiliano makali kuhusu hatima yake.
Katika mradi huo ingawa mazungumzo ya awali ulikuwa upitie katika Bandari ambayo bado inajengwa ya Lamu, Kenya hadi Uganda, hali hiyo inaonekana kushindikana baada ya suala la usalama, miongoni mwa mengine mengi, kujitokeza na Serikali ya Kenya kukosa majibu.
Kutokana na sababu hiyo na kusuasua kwa mradi huo, Serikali ya Uganda iliamua kugeukia Tanzania ambako kwa haraka mkataba wa awali ulisainiwa mjini Arusha na maandamizi kuanza ambapo bomba hilo litaanzia Bandari ya asili ya Tanga hadi Uganda.
Hata hivyo tangu kusainiwa kwa makubaliano ya mradi huo kujengwa Tanzania, kumekuwa na harakati nyingi kwa upande wa Kenya kujaribu “kupambana” kuurejesha mradi huo. Ni mapambano haya ambayo sasa yamezua mijadala mingi katika vyombo vya habari na mitaani.
Nikiwa mtaalamu wa eneo hili, bila kujali utaifa, nashawisha kusema Nairobi iache kufanya siasa katika suala hili la kitaalamu na wala haihitajiki propaganda yoyote katika ukweli uliodhahiri. Sababu hizi 10 zinainyima Nairobi haja na hoja ya kuwa mwenyeji wa mradi huo.
#1 Usalama
Jambo moja la kuamua mradi huu ujengwe wapi na ambalo haliwezi kupuuzwa ni usalama. Eneo ambako Kenya wanashadidia mradi huo upite la Kaskazini mwa nchi hii linafahamika kwa changamoto za kiusalama na hakuna uhakika mtu anaoweza kuutoa.
Eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo yako karibu na ngome za wapiganaji wa Al-Shaabab kiasi kwamba mjenzi yeyote wa mradi huo hawezi kuhatarisha usalama wake na wa bomba hilo katika siku zijazo.
Nimeshangazwa kumuona Rais Uhuru Kenyatta licha ya ukweli huu akizidi kupambana na kujitutumua. Ni suala lililowazi kuwa kujenga bomba hilo katika ukanda huo ni kuwapa fursa nyingine rahisi magaidi wa Al Shaabab kupata eneo jingine la mashambulizi yao. Katika hili siwezi kuiunga mkono Nairobi hata kama mimi ni Mnairobi.
#2 Jiografia
Wataalamu wa jiografia ya eneo la mpaka wa Kenya na Uganda pia wanaeleza changamoto ya milima ambayo itakuwa na athari kubwa katika gharama za kusukuma mafuta hayo kutoka Uganda kuja eneo la Kenya.
Uozefu wa bomba la mafuta la Tazama linaloanzia Tanzania na kupita nyanda za juu za Iringa na Mbeya kabla ya kufika Zambia unaonesha ukweli wa hili. Hii inaweza kuyafanya mafuta ya Uganda kuwa ghali hasa wakati huu ambapo bei ya mafuta imeshuka duniani na kujikuta yakikosa soko.
Akifafanua hili mmoja wa wahandisi wanaofahamu gharama kubwa za Tazama katika kuyavusha mafuta nyanda za juu anasema:
“Kupitishia bomba hilo nyanda za juu kama zile za mpaka wa Kenya na Uganda kutaibua changamoto nyingine mpya ya kulazimika ama kujengwa vituo vya umeme au mradi kuongezeka gharama zaidi kwa kuweka majenereta ya umeme. Sisi Tanzania tuna uzoefu wa gharama hizo kwa bomba la Tazama.”
#3 Aina ya mafuta
Katika ziara kadhaa za kikazi nchini Uganda nimepata fursa ya kufanya mahojiano na wataalamu wengi walioko katika sekta ya mafuta nchini humo. Hapa kuna ukweli ambao unamfanya Rais Kenyatta aukubali.
Tunaelezwa na wataalamu hao kwamba mafuta yanayopatikana Uganda ni mazito na yana ganda haraka sana. Hii inaaongeza changamoto nyingine kubwa kwa upande wa Kenya. Ukanda linakotakiwa kupita bomba hilo ni wa juu na wenye hali ya ubaridi. Hii itasababisha mafuta hayo kuganda na kuhitajika gharama kubwa zaidi ya kulipasha joto bomba hilo.
“Hii itasababisha hata teknolojia yenyewe ya ujenzi wa bomba kuwa tofauti na ndio maana ukisikia gharama za kulipitisha Kenya ambako njia kidogo ni fupi bado zinakuwa kubwa kuliko likipita Tanzania ambako njia kidogo ni ndefu lakini gharama zitakuwa ndogo,” anasema mmoja wa wataalamu wa nishati hapa Nairobi.
# 4 Gharama kubwa
Nimedokeza hapo awali kuwa wataalamu wamekadiria kuwa gharama za kupitisha bomba hilo njia ya Kaskazini mwa Kenya, licha ya changamoto za kiusalama, bado zitakuwa kubwa sana. Kutoka Bandari inayotarajiwa kujengwa ya Lamu hadi Uganda ni takribani kilometa 1,300 hivi lakini ujenzi pekee utagharimu dola za Marekani bilioni 4.5.
Ujenzi kama huo iwapo utafanyika kwa njia ya Tanzania ambayo inafikia kilometa 1,400 hivi utagharimu dola za Marekani bilioni 4.0. Hii ni sawa na kusema Serikali ya Uganda itapata punguzo la zaidi ya Sh. Trilioni moja za Kitanzania (dola za Marekani milioni 500) kwa njia ya Tanzania.
#5 Ufadhili
Suala la fedha za ujenzi wa mradi huu nalo ni la muhimu kulitazama kwa kina na mapana yake. Si Serikali ya Uganda, Kenya wala Tanzania yenye fedha zake yenyewe za kujenga mradi huo. Uganda hasa mwenye mradi huo ndiye anategemewa kusaka wafadhili au kutumia aliokwishakubaliana nao.
Wakati Kenya wanasubiri kuanza kusaka mfadhili wa ujenzi huo iwapo watafanikiwa kuurejesha, Tanzania na Uganda zimeshamaliza utata wa eneo hilo. Kampuni ya Total ya Ufaransa imeahidi kufadhili ujenzi kwa kutumia Dola milioni 4 katika ujenzi huo.
Na si tu ufadhili huo umeshatolea lakini tunaambiwa pia wataalamu wa Tanzania wakiongozwa na mabingwa wao wa kusimamia miradi kama hiyo ya mabomba na wenye uzoefu wameshatoa kalenda ya utekelezaji na kukubaliana na Total. Hapa Nairobi tunataka nini zaidi.
# 6 Uzoefu
Nafahamu kwamba Kenya wanayo miradi kadhaa ya mabomba ya mafuta lakini tukubali kuwa kama kuna nchi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ina uzoefu kuhusu ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa mabomba ya mafuta na gesi basi ni Tanzania.
Tangu miaka ya 70 Tanzania imekuwa, kwa kushirikiana na Zambia, ikiendesha bomba la mafuta la Tazama ambalo linaanzia katika Bandari ya Dar es Salama kwenda Zambia. Kana kwamba hiyo haitoshi, Tanzania imekuwa ikisimamia miradi ya mabomba ya gesi kuanzia lile la Songosongo hadi la sasa la Mtwara-Dar es Salaam.
Mabomba yote haya pia katika muda wote huo yameendeshwa katika hali ya usalama bila kuwepo kitisho chochote cha kiusalama licha ya Tanzania kupita katika kipindi kigumu (kwa bomba la mafuta) cha kusaidia harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika huko nyuma.
# 7 Siasa
Siasa ni suala muhimu katika hili. Wakati Tanzania si tu ina hali ya amani na utulivu lakini siasa zake zinatabirika. Ripoti mbalimbali za utawala bora na siasa Barani Afrika zinaitaja Tanzania kuwa nchi ambayo viongozi wake wanarithishana madaraka kwa amani.
Kenya imeushindwa mtihani huu. Mauaji na vurugu kubwa zilizoibuka mwaka 2007/08 ni ushuhuda wa kutotabirika kwa utulivu wa kisiasa nchini humo. Hakuna mwekezaji anayeweza kuwekeza katika nchi yenye siasa zisizotabirika.
Lakini pia kwa sasa ujio wa Rais John Pombe Magufuli: mwanasiasa wa aina yake anayataka kuona mambo yakienda na kukamilika kwa haraka, bila shaka, kimekuwa kivutio kwa Rais Museveni anayatamani aanze kusafirisha mafuta hayo hata leo kwa faida ya wananchi wake.
# 8 Muda wa Ujenzi
Nimegusia hapo awali kama kuna kitu kinamuumiza kichwa kwa sasa Rais Museveni ni kuchelewa kwa mradi huu. Itakumbukwa kuwa mkataba wa awali wa makubaliano na Nairobi ulifanyika 2014: miaka miwili baadaye hakuna kilichofanyika.
Juzi Mzee Museveni amesaini mkataba wa makubaliano na Rais Magufuli, ndani ya mwezi mmoja Rais wa Total amewasilisha mpango wa utekelezaji kwa Rais Magufuli ambaye naye ametoa maoni na baraka zake na sasa hatua nyingine zitachukua nafasi yake.
Hii ina maana kuwa Tanzania iko tayari kuipa Uganda thamani nyingine muhimu katika ujenzi huu: muda mfupi wa kukamilisha ujenzi huo kitu ambacho Nairobi imekichezea kwa miaka miwili iliyopita.
# 9 Sakata la Kabila la Waacholi
Hili halisemwi sana lakini lipo na ni changamoto kubwa katika kujenga bomba hilo kwa njia ambayo Nairobi wanaitaka. Katika eneo wanakotaka bomba kupita linagusa eneo la msitu wa asili wa kabila la Waacholi.
Msitu huo kwa mujibu wa mila za kabila hilo ni maalum kwa ajili ya kuwinda na sehemu ya tamaduni zao. Hawa mara kadhaa wameibuka kupinga hilo ingawa hawajapewa uzito.
Museveni kwa aina ya utamaduni wa Uganda wa kuheshimu mila na desturi za makabila muhimu kama vile Wabaganda na hili la Waacholi, bila shaka, na naamini hivyo hawezi kuingia katika mgogoro wa kikabila unaoweza kuepukika.
# 10 Ni Tanga au Lamu?
Hii nayo kama ilivyo hoja niliyoanza nayo ya usalama ni hoja ya mwisho lakini si ya mwisho kwa umuhimu. Nimeeleza hapo awali kwamba Uganda wameumizwa sana na bila shaka wamehuzunika pia ujenzi huu kuchelewa.
Sasa kama kuna kituko na kitu kingine kitakachowaumiza sana Waganda ni shere wanayotaka kuchezewa na Nairobi yangu. Taarifa nilizonazo ni kwamba mpaka sasa unaposoma makala haya Bandari wanayoitaja kuwa mwanzo wa bomba husika ya Lamu ni kama haipo: ndio kwanza inajengwa!
Pili hata itakapokamilika Bandari hiyo ambayo imeanza kukumbwa na matatizo ya fedha za ufadhili wake tofauti na ile ya asili na iliyozungukwa na visiwa ya Tanga, itakuwa na changamoto kubwa ya mawimbi ya bahari kiasi cha kuzifanya meli kutia nanga kwa shida. Baadhi ya wataalamu wanasema hilo litaiongezea Uganda gharama ya kujenga matenki mengi ya kuhifadhi mafuta nje ya bandari hiyo ya Lamu na kuongeza gharama nyingine nyingi.
Wakati Lamu ikiwa hivyo na ujenzi wake ukiwa bado unasuasua (mpaka sasa hata gati moja halijakamilika), Bandari ya Tanga litakakoanzia bomba hilo kwa Tanzania, inafanyakazi, imewavutia Waganda wenyewe walipoitembelea juzi na ipo eneo tulivu lisilo na mawimbi.
Sasa kwa sababu kama hizi hakuna sababu ya sisi wa Nairobi kuanza kuhaha huku na kule au kuanza kutumia wanaharakati eti kudai bomba litapita Serengeti (ambayo kwa mujibu wa ramani rasmi si kweli, linapita mbali kabisa katika mkoa wa Geita), ushauri wangu kwa Kenyatta ni atumie nguvu nyingi kushughulikia kwanza ujenzi wa Bandari ya Lamu ukamilike.
Wasalaam wana Afrika Mashariki.
*Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni raia wa Afrika Mashariki anayefuatilia kwa karibu sekta za mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.