UNAWEZA kutumia muda mrefu kumtafuta na pengine usimuone kijana mmoja anayeitwa Ali Saleh, lakini ikakuchukua sekunde chache tu kumpata Ali Kiba, yule nyota wa muziki wa kizazi kipya, aliyeibuka na kibao cha Cinderela miaka kadhaa iliyopita.
Yuko katika game kitambo sasa na kazi zake nyingi zinafahamika, hasa kwa kuwa amethibitisha pasipo shaka kwamba anao uwezo mkubwa wa kuimba.
Hivi karibuni Ali Kiba aliteuliwa kuwa mmoja wa mabalozi wa kampeni kubwa inayofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii nchini, ya kupinga uwindaji haramu wa wanyama pori, hasa tembo, unaofanywa na majangili katika mbuga na hifadhi mbalimbali.
Kampeni hiyo inaihusisha asasi ya kimataifa ya WildAid pamoja na African Wildlife Foundation, ambazo zimeamua kushirikiana na wizara kuhakikisha mnyama tembo ananusurika, maana jinsi anavyotafutwa na kuuawa, ni jambo la kusikitisha sana. Kwa hapa nchini, sambamba na Ali Kiba, balozi mwingine ni Jacqueline Mengi, mwimbaji wa zamani na Miss Tanzania mwaka 2000 maarufu kama K- Lynn.
Asasi hiyo ya kimataifa inao pia mabalozi wengine ambao ni wasanii na mastaa maarufu duniani, akiwemo David Beckham, , Leonardo Di Caprio, Prince William, , Jackie Chan na Lupita Nyong’o.
Juzikati, Ali Kiba aliwalalamikia Wabongo, kwamba pamoja na kupewa ubalozi huo, tena akiwa na mastaa hao, bado mapokeo yake yamekuwa madogo mno, tofauti na matarajio yake. Ni ubalozi wa kazi kubwa, akiwa na mastaa wakubwa, hivyo alitegemea habari hiyo kupewa ukubwa unaostahili!
Anasema Wabongo siyo watu wa kusifia vitu vizuri hasa vinavyofanywa na Wabongo wenzao, kazi yao kubwa ni kutafuta dosari na kuitolea macho, kama alivyotoa mfano wa jinsi marehemu Steven Kanumba alivyoboronga lugha ndani ya jumba la Big Brother Africa, kwani watu waliijadili zaidi hiyo badala ya kusifia uwakilishi wa mtu wao mjengoni!
Ingawa kiukweli haikai sawa, lakini sidhani kama Ali Kiba ni mtu wa kutegemea majina ya watu wengine ili kumfanya kuwa habari kubwa. Anawajua Wabongo ambao kusifia cha kwao, siyo zao!
Lakini licha ya tabia hizo zisizofaa za Wabongo, kwani hawa ni mastaa wa kwanza Ali Kiba kukutana nao kwenye ‘project’ kubwa? Nadhani jambo la msingi ni kuwa nini mtu unafanya unapokutana na mtu anayeweza kukupa fursa, na siyo ukubwa wa jina lake.
Katika mradi wa One 8 uliofadhiliwa na Airtel mwaka 2010, Ali Kiba alikutana na mkali wa R&B duniani, R Kelly, Mkongo Fally Ipupa na wakali wengine wa Afrika kutengeneza kibao kilichoitwa Hands Across the World. Habari zake zilipaa huku na kule, kiasi kwamba hapa nyumbani, alikuwa ndiyo habari ya ‘mujini’.
Nini kilifuata? Recognition haiwezi kuja kwa sababu ya unayeambatana naye, bali unachokifanya ukiwa naye. Kama alishindwa kutumia fursa ile kutanua muziki wake Afrika na Marekani, leo David Beckham atamsaidia nini? ‘Midia’ impe ‘coverage’ kubwa kwa kuwa yupo meza moja na mzee Jackie Chan?
Tuthamini vya kwetu, lakini mastaa wetu nao watuheshimu, wasituone ni watu rahisi kudanganyika kwa kutumia migongo ya watu wengine.
GPL