

Akiongea katika kikao kazi cha watumishi wa TARURA wa Mradi wa RISE pamoja na Wawakilishi wa Benki ya Dunia, kilichofanyika leo jumanne tarehe 05/03/2024 mwakilishi wa Benki ya Dunia Mhandisi Yonas Mchomvu amesema wao kama Benki ya Dunia wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa RISE ambapo wamempongeza Mtendaji Mkuu wa TARURA kwa kuendelea kusimamia vyema Miradi inayotekelezwa na Serikali kwa Ufadhili wa Benki ya Dunia pia aliipongeza TARURA kwa kuwa na mpangilio mzuri wa wataalamu wa kuendesha mradi ikiwa ni pamoja na kuwa na Kitengo cha Mazingira na Jamii.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff (pichani) akizungumza katika kikao kazi hicho ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya Barabara inayotekelezwa chini ya TARURA Nchini.
Akizungumza katika kikao hicho mratibu wa Miradi ya Benki ya Dunia toka TARURA Mhandisi Haumprey Kanyenye (mwenye tai nyeusi) amesema Mradi wa RISE ulianza Novemba 2021 na utakamilika Juni 2027. Mradi wa RISE umelenga kujenga jumla ya kilometa 535 za barabara kwa kiwango cha lami, kujenga maeneo korofi ya barabara ili yapitike, na kufanya matengenezo ya barabara ya jumla ya kilometa 23,000km kwa kuwashirikisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara husika . Aidha, Mhandisi Kanyenye alieleza uchaguzi wa Mikoa, Wilaya na barabara ambapo Mradi wa RISE unatekelezwa ulizingatia maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo kutoka kwenye Mpango wa Maendeleo wa Kilimo (ASDPII).






