Katibu Mkuu ofisi ya Rais-Ikulu -Dr. Moses Kusiluka ametoa wito kwa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuondokana na umaskini uliokithiri.
Dr. Kusiluka ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipotembelea na kukutana na baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kukagua miradi inayotekelezwa na TASAF katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha ambako aliambatana pia na baadhi ya Wajumbe wa bodi .
Amesema Serikali inatambua changamoto ya Umaskini unaowakabili wananchi ,lakini akasisitiza kuwa ili kuitokomeza changamoto hiyo wananchi wanapaswa kujituma kwa kufanyakazi kwa bidii na maarifa na kutumia vizuri mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kuinua mapato yao.
Aidha Dr. Kusiluka amehimiza wazazi kutilia mkazo suala la elimu kwa watoto wao ambao amesema Hiyo ndiyo njia ya uhakika ya kujenga jamii bora ya baadaye itakayoleta ukombozi wa kweli wa ujenzi wa uchumi thabiti wa kaya husika na taifa kwa ujumla huku ikikemea vikali vitendo vyovyote vinavyoathiri maendeleo ya wanafunzi hususani watoto wa kike.
‘’tumieni vizuri fursa mliyoipata ya kuwa shuleni ili mtimize ndoto zenu za kuwa wataalamu wa fani mnazozitaka katika utumishi wa taifa hapo baadaye’’ alisisitiza Dr. Kusiluka baada ya kukagua nyumba na hosteli ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari ya Khusumay ambayo yamejengwa na TASAF.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Bodi ya taifa ya Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Shughuli za Mfuko huo , Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa Mfuko huo unaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kusaidia jitihada za kupunguza umaskini nchini.
Wakiwa katika kijiji cha Khusumay,Wajumbe hao wa bodi ya taifa ya Uongozi ya TASAF ,walitembelea kaya za baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kujionea namna walengwa hao walivyofanikiwa kuboresha makazi yao, kununua mifugo hususani mbuzi, ng’ombe ,kuku na nguruwe kwa kutumia ruzuku waliyoipata kutoka TASAF kama njia mojawapo ya kukuza uchumi wa kaya za Walengwa hao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- Bw. Ladislaus Mwamanga ameishukuru serikali kwa kuendelea kuuthamini Mfuko huo na kuridhia utekelezaji wake kuendelea katika sehemu ya pili ambayo amesema imeagizwa kutekelezwa katika maeneo yote nchini.
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/34WLFuy
via







