Na Leandra Gabriel, Michuzi Tv
KATIKA kuadhimisha maonesho ya 43 ya biashara maarufu Kama sabasaba Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA)wamejizatiti katika kuendana na kasi ya awamu ya tano ambayo kwa kiasi kikubwa imejikita zaidi katika kujenga uchumi wa viwanda na kulipeleka taifa katika uchumi wa Kati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Michuzi Tv mara baada ya kuwatembelea katika banda lao la maonesho katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam, wadau mbalimbali wameeleza namna VETA inavyoshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuchangia ukuaji wa kiuchumi hasa kwa kuzalisha vijana waliobobea katika fani mbalimbali.
Akieleza namna wanavyoshiriki katika shughuli za kilimo Gema Ngoo ambaye ni mkufunzi wa masomo ya kilimo amesema kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali juu ya kilimo bora na cha kisasa zaidi ili kuweza kuzalisha mazao yanayoendana na soko kwa Sasa.
“Maarifa mengi yanatolewa kwa vijana na sio katika kilimo pekee pia na namna ya kupambana na wanyama waharibifu, hapa tuna ndege aina ya tai ambaye ametengenezwa kitaalamu na anaweza kutembea takribani katika hekta kumi kufukuza wanyama waharibifu, pia tuna mafunzo ya umeme, upishi, useremala na vingine vingi” ameeleza Ngoo.
Aidha amesema kuwa VETA wataendelea kushirikiana na serikali na taasisi nyingine ili kuhakikisha azma ya serikali ya awamu ya tano inafikiwa na amewataka vijana kutembelea katika banda lao ili waweze kupata ujuzi wa namna ya kujiajiri wenyewe.
Vilevile William Mnuo ambaye ni mkufunzi wa magari hasa magari makubwa yakiwemo mabasi ameeleza kuwa wapo makini katika kuhakikisha wataalamu hasa madereva wanaozalishwa kutoka VETA wanakuwa wa mfano na mabalozi bora kwa wenzao.
Mnuo amesema kuwa maarifa na ustadi unaotolewa na VETA kote nchini umelenga katika kuwakomboa vijana kutoka katika mawazo ya kuajiriwa na kuweza kujiajiri wenyewe.
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/3035RI7
via




