Wiki
hii kama kawaida nazungumzia mada inayogusa maisha yetu ya kimapenzi,
si unajua bila mapenzi hakuna maisha! Huo ndiyo ukweli, huwezi kuishi
kama jiwe au mti. Raha ya maisha ni kuwa na mpenzi wa kumpenda na yeye
akakupenda kiukweli na siyo kuigiza kama ilivyo kwa baadhi ya watu.
Kwa
wale walio katika mapenzi matamu na ya kweli watakubaliana na mimi kuwa
mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama ‘kapepo’ kadogo ndani ya
ulimwengu huu mkubwa uliojaa vituko!
Wakati
wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo
wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa! Kila siku ni
karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao japo wanawapenda
sana na kuonesha mapenzi yao yote.
Kila siku ni maumivu na simanzi ya moyo isiyojulikana hatima yake.
Lakini
pamoja na karaha, vituko na dharau zinazofanywa na wale tuwapendao,
bado kuna ambao wamejaaliwa mioyo ya uvumilivu. Hawa ni wale wanaoamini
ule msemo usemao, subira yavuta heri. Yaani wanaamini ipo siku wapenzi
wao watabadilika na maisha yatakuwa matamu.
Ni
kweli kuna wanaofanikiwa katika hili lakini wapo ambao uvumilivu wao
unapitiliza. Ndugu zangu, kila kitu kina kikomo, kama umevumilia kwa
muda mrefu lakini ukaona hakuna mabadiliko, uamuzi sahihi ni ‘kusitisha
safari’.
Lakini
kama una moyo wa chuma na huumizwi na yale mabaya anayokufanyia mpenzi
wako, hakuna anayeweza kukulazimisha umuache. Watu watakuangalia na
kuishia kukuonea huruma tu.
Labda
unaweza kujiuliza ni kwa nini baadhi wanavumilia mabaya wanayotendewa
na wapenzi wao? Iko hivi, yawezekana anayevumilia anahisi huyo aliyenaye
ndiye mtu sahihi na anaamini akimuacha atampata mwenye mateso zaidi,
hivyo anaona amvumilie huyo aliyemzoea.
Lakini
wengine ni ulimbukeni tu, yaani wao wanahisi hayo ndiyo maisha.
Kutukanwa, kupigwa, kusalitiwa na kufanyiwa mambo mengine ya namna hiyo
ni sehemu ya maisha. Yaani wanaamini si wao tu bali hata kwa wengine ni
hivyohivyo. Mh!
Lakini
sasa kuna hili suala la kukosewa na mpenzi wako kisha akakuomba
samahani. Hili katika mapenzi linakubalika kabisa kwani kila siku
tunakoseana na samahani ndilo neno linaloweza kurudisha amani katika
penzi.
Kuna
watu ni wagumu sana kuomba msamaha. Yaani wanajua wamekosa lakini
wanaona kuomba msamaha ni kujishusha. Hii ni mbaya sana na inaweza
kusababisha kupunguza mapenzi kati ya wawili waliotokea kupendana.
Pia
kuna ambao ni wagumu kusamehe. Yaani mpenzi wake kafanya kosa kwa
bahati mbaya na anagundua amekosea lakini akiomba msamaha, hasamehewi.
Hili nalo ni tatizo!
Ila sasa kuna watu ambao kila siku ni samahani tu. Wapo ambao kila siku wanakosewa na wapenzi wao na kuishia kuombwa msamaha.
Hili kimsingi ni jambo linaloweza kuleta picha ya tofauti.
Tunachojua
ni kwamba, unafanya kosa leo, unaomba msamaha na kutorudia tena kosa.
Lakini kama leo unamsaliti mwenzako, anakusamahe, kesho tena unasaliti,
kwa kuwa anakupenda anakusamehe, keshokutwa tena unarudia kosa lilelile,
katika mazingira hayo ni kweli unastahili kuendelea kusamehe?
Sidhani
kama inakuja! Kurudia makosa yaleyale kwa kutarajia kuwa utaomba
msamaha na kusamehewa ni kuonesha kwamba unamdharau mwenzio na kimsingi
kama utakuwa ni mtu wa ‘am sorry dear’ kila siku na hubadiliki, hiyo ‘am
sorry’ yako haitakuwa na faida.
Ninachoweza
kusema ni kwamba, kama huyo uliyenaye unampenda kwa dhati, anaweza
kukukosea mara nyingi kwa makosa mbalimbali na ukaendelea kumsamehe bila
kuchoka kwa kuwa unampenda na hauko tayari kumkosa kwa makosa
yanayosameheka.
Lakini
kama mpenzi wako atakukosea makosa mawili-matatu kisha ukafanya uamuzi
wa kumuacha, utakuwa unadhihirisha kwamba, hukuwa na mapenzi ya dhati
kwake na ndiyo maana kakukosea mara moja au mbili, ukaona ndiyo mwanya
wa kumpiga kibuti.
Tujenge utamaduni wa kusameheana kwani hakuna aliyekamilika kwa asilimia 100 na ndiyo maana kila siku tunakoseana.