Na Charles James, Michuzi TV
Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Dodoma Mjini kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 kwa kuwafikia na kutatua kero,matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wake na pia kuwasimamia Viongozi wote wachaguliwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCMbna kutatua matatizo ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Robert Mwinje wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya uenezi (Spika) na bendera kwa kata zote 41 vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Tunataka viongozi wote mliopo Serikalini na wawakikishi wa wananchi mnaotokana na CCM kuhakikisha mnatatua matatizo ya wananchi kuanzia ngazi ya chini kabisa ili tutengeneze uhalali kwa wananchi kuja kuwaomba ridhaa mwaka huu 2019 na mwakani 2020” amesema Mwinje
Akitoa maelezo ya awali,Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe Mavunde amesema kwamba vifaa hivyo alivyotoa leo kwa kila kata na Uongozi wa Wilaya wa Jumuiya Spika 45 zenye thamani ya Tsh 16,000,000 na bendera 1000 zenye thamani ya Tsh 3,500,000 ni maandalizi ya kampeni ya kisayansi ambayo wamepanga kuifanya katika Jimbo la Dodoma ili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi huu wa serikali za Mitaa.
“Kupendeza kwetu kwa mashati ya kijani na kuimba kwetu vizuri nyimbo za CCM hakuna maana kama hatutakua Chama cha kujibu kero za wananchi. Nimejipanga vizuri kuhakikisha naendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuhakikisha Jimbo la Dodoma Mjini linaendelea kutoa kura nyingi kwa CCM katika uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka 2020.Rais Magufuli na CCM imetufanyia mambo makubwa sana hapa Dodoma hususani Jimbo la Dodoma Mjini shukrani yetu tutailipa kwenye sanduku la kura” amesema Mavunde
Wakati huo huo, Mbunge Mavunde ameahidi kutoa Tsh 20,500,000 kwa mgawanyo wa Tsh 500,000 kwa kata zote 41 katika kutunisha mfuko wa Uchaguzi wa Kata. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi wa Chama Wilaya na Viongozi wa Chama na Jumuiya zote kwa ngazi ya kata zote kwa Jimbo la Dodoma Mjini pamoja na Madiwani wa Kata na Viti Maalum.
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2YSiN3D
via