Tukio hilo la majonzi lilijiri kwenye Hospitali ya Bugando mkoani hapa
ambapo wasanii hao walikwenda kumfariji mama wa mtoto huyo aliyetekwa
mjini Geita hivi karibuni.
Walipofika wodini hapo, JB na wenzake walitoa yao ya moyoni kupinga
vikali ukatili aliotendewa mama huyo na mwanaye huku wakitahadharisha
juu ya laana inayoweza kuikumba jamii yetu kwa tukio hilo.
JB: Nampa pole sana mama Yohana. Hii ni aibu kubwa kwa taifa letu na jamii pana duniani.
Watu hawafanyi kazi kujipatia kipato halali. Mafisadi wanataka kujipatia
fedha kupitia njia za kishetani za kuwaua wenzetu. Albino ni wenzetu na
tunawapenda. Lazima wahalifu wakamatwe na wahukumiwe kunyongwa.
Mzee Majuto: Inasikitisha sana. Haivumiliki. Albino ni wenzetu na wana
uwezo mkubwa wa kulisaidia taifa letu. Wahusila lazima wakamatwe na
tuone wakichukuliwa hatua kali.
Richie: Natokwa na machozi. Hiki ni nini? Hatuwezi kufumbia macho jambo
hili hasa sisi wenye nafasi kubwa ya kukemea vitendo hivi.
Mara baada ya mastaa hao kutoa la moyoni katika wodi aliyolazwa mama
huyo, iligeuka kama msiba kwani kila aliyekuwepo alikuwa akiangua kilio
kwa uchungu.
Tayari mtoto Bahati amezikwa baada ya mwili wake kupatikana ukiwa hauna
baadhi ya viungo huku mama yake akiendelea na matibabu baada ya
kufanyiwa oparesheni sehemu ya kichwani aliyojeruhiwa vibaya wakati
akinyang’anywa mwanaye.
Tunampa pole sana mama Yohana Bahati, watanzania tuungane kupinga ukatili huu.
GPL