Miaka ya 1970 baadhi bendi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) zilivamia soko la muziki humu nchini zikiporomosha muziki.
Ikumbukwe mwaka 1973, Franco Luambo Luanzo Makiadi akiwa na bendi yake ya T.P. OK. Jazz alikuja hapa nchini na akafanya onyesho kamambe katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwaka mmoja baadae wa 1972 bendi ya Maquis du Zaire, nayo ikaingia kwa mbwembwe na kuweka makazi yake ya kudumu katika jiji la Dar es Salaam.
Makala hii inaizungumzia bendi hiyo ambayo âiliwatesaâ baadhi ya Watanzania wapenda muziki wa dansi kwa kuwaporomoshea burudani ya muziki katika kumbi mbalimbali hapa nchini.
Bendi hiyo ni Maquis du Zaire, iliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikafia humu nchini miaka 1990.Ili kuipata historia kamili ya bendi hiyo mwaka 1981, nilifanikiwa kufanya mahojiano maalum na mmoja wa waliokuwa viongozi wa bendi hiyo Chimbwiza Mbangu âNguza Vickingâ.
Alisimulia kwa kina wasifu wa bendi hiyo akisema kwamba mwaka 1960, vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), waliungana na kuunda bendi yao wakaiita Super Theo.
Nguza alisema kuwa bendi hiyo ilikuwa ikitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki wa mji huo wa Kamina na vitongoji vinavyouzunguka mji huo.Alisema baadae wakaibadilisha majina ya bendi ikawa Super Gabby. Lakini uongozi wa Super Gabby ulitaka kuleta mageuzi katika muziko, mwaka 1972, wakabadilisha majina rasmi kuwa Maquis du Zaire.
Mwaka huohuo bendi hiyo iliingia hapa Tanzania wakapitia nchini Uganda.
Walipofika katika jiji la Dar es Salaam walipata mkataba wa kupiga muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa maeneo la Tazara Buguruni jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza mkataba wao waliondoka wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa kipindi kifupi.
Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima, aliyekuwa akimiliki wa ukumbi wa Safari Resort maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam. Wakaanza kupiga muziki kwa mkataba na mfanyabiashara huyo.
Februari 1977 viongozi wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire, waliamua kukiongezea nguvu kikosi chao. Hivyo walimtuma Tchibangu Katayi âMzee Paulâ aliyekuwa mwanamuziki wa bendi ya Maquis du Zaire. Pia alikuwa mmoja kati ya viongozi wa bendi hiyo.Mzee Paul aliwachukua baadhi ya wanamuziki ili kuja Tanzania kuongeza nguvu katika bendi ya Maquis du Zaire.
âMzee Paulâ alibahatika kuwachukuwa wanamuziki akina Kikumbi Mwanza Mpango âKing Kikiâ, mtunzi na mwimbaji, Kanku Kelly kwa upande wa tarumbeta., Ilunga Banza âMchafuâ, aliyekuwa akiungurumisha gitaa la besi, Mutombo Sozy aliyekuwa akizicharanga drums, na mnenguaji Ngalula Tshiandanda.
Wakati huo Maquis du Zaire walikuwa wakicheza muziki wakitumia mtindo wa âChakula Kapombeâ, ambao kwa Watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na mashabiki.
Kufika kwa wanamuziki hao kulileta changamoto kubwa katika muziki. Tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango âKing Kikiâ, zilikuwa chachu masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Kiki pia yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta Mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.
Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa âKamanyolaâ uliowapagaisha wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es Salaam.
Mwishoni mwa 1977, Marquis du Zaire, walimaliza mkataba kwa Hugo Kisima, wakaondoka.Bahati nyingine ikawadondokea tena baada kuingia mkataba mwingine wa kupiga muziki kwa mzee Makao, aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah, maeneo ya Ubungo.Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya âSanifuâ na âOgelea piga mbiziâ.
Lakini ukumbi huo ukabadilishwa jina ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba Maquis pia ilikuwa ikipiga kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge.Mwishoni mwaka Maquis du Zaire 1978 waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka DRC.Iliwaleta akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na Khatibu Iteyi Iteyi.
Bendi hiyo ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza âChichiâ, Chibangu Katayi âMzee Paulâ, Chimbwiza Mbangu Nguza âNguza Vickingâ, Mutombo Lufungula âAudaxâ na Mbuya Makonga âAdiosâ.
Chini ya uongozi huo, miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana, mojawapo ni lile la kuanzisha Kampuni iliyofahamika kama Orchestra Maquis Company (OMACO).
Kampuni hiyo iliweza kumiliki shamba la matunda, wakalima kwa kutumia treka zao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.OMACO pia ilimiliki mradi mwingine wa viwanja tisa na nyumba kadhaa, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Aidha iliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.Vijana wa wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu kila siku za Jumamosi.Waliwashuhudia wanamuziki wa bendi hiyo waliokuwa watanashati, nidhamu ya hali ya juu hususan wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.
Enzi hizo ilikuwa ukiingia katika ukumbi huo wa White House, mbele yako macho lazima yakutane na mbao zilizokomelewa juu ya mwembe uliokuwa ukumbini hapo, zikiwa zimenakshiwa kwa maandishi ya majina ya wanamuziki wote.
Maquis du Zaire ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha muziki kwa muda na kusikika kipaza sauti kikiuliza âWapenzi mumekuja na miswakii? Wapenzi walikuwa wakijibu ândiyoooâŠâ Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo.
Watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani kwani muziki wa Maquis du Zaire, ulikuwa unarindima hadi alfajiri. Muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi. Wakati huo hazikuwepo âDala dalaâ, Bajaji wala Pikipiki.
Kupitia ubunifu waliokuwa nao wanamuziki hao waliweza kubadilisha mitindo mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya âChakula kapombeâ, âKamanyolaâ, âSanifuâ, âBishe Bisheâ, âZembwelaâ, âChekechaâ na Ogelea Piga mbizi.
Mpulizaji wa Tarumbeta Mwema Mudjanga âMzee Chekechaâ alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake ukumbini humo akitoa
Alikuwa Mwema Mudjanga âMzee Chekechaâ aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo ukumbini. Licha ya kazi yake ya kupuliza tarumbeta, aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia vibwagizo vya âChekeeeâŠ. Chekechaaaâ âCheza Kamanyola bila jashoâŠâ, âTusangalaaâ, âAima imaaâ, âBishe bisheeâ, âSaa⊠Sanifuuâ, âcheza Kamanyolaaâ âcheza kwa maringoâ, â Cheza ukijidaiâ na mengine mengi.
Maquis du Zaire wakati huo ilikuwa imesheheni wanamuziki takriban 40, wenye talanta zinazopishana.Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.Mpendwa msomaji naomba nikujuze au kukumbusha kikosi kamili kilichokuwa kinatengeneza bendi hiyo kwa nyakati tofauti.
Safu ya waimbaji walikuwepo akina Kikumbi Mwanza Mpango âKing Kikiâ, Mbuya Makonga âAdiosâ, Mutombo Lufungula âAudaxâ, Mukumbule Lolembo âParashiâ, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na Kyanga Songa.
Wengine walikuwa Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda âClaytonâ, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Masiya Radi âDibakuba kubaâ, Issa Nundu na waimbaji wa kike Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.
Wapiga gitaa la solo alikuwepo Chimbwiza Nguza Mbangu âNguza Vickingâ, ambaye kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo, wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha âField Marshalâ.Wengine katika gitaa hilo walikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga âVumbiâ, na Mbwana Suleiman âMbwana Coxâ.
Gitaa la rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji âVataâ, Omari Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Halikadharika walikuwepo akina Mbambu Kazadi, Mondo Mondonde na Nawayi Kabwila.
Kwa upande wa uungurumishaji wa gitaa zito la besi walikuwa akina Ilunga Banza âBanza Mchafuâ ambaye aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kulimudu gitaa hilo akiwa kajitwisha kwenye upara uliozungushiwa simbi kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.
Kwa upande wa wapuliza Saxophone âmdomo ya bataâ walikuwepo akina Mafumu Bilali âBombengaâ auâSuper Saxâ, Khatibu Iteyi Iteyi, Kalamzoo, Alex Kanyimbo, Akulyake Suleimani âKing Malluâ, Roy Mukuna âMukuna wa Mukunaâ, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na Majengo Selemani.
Wapulizaji tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga âMzee Chekechaâ Nkashama Kanku Kelly, Mioma wa Mwamba âMzee Titoâ, Kayembe Ndalabuu âTrumblooâ, Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde, Kaumba Kalemba, Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi âBizosâ, Morgan Machege na Ngenda Kalonga.
Pamoja na uimbaji Mbuya Makonga âAdiosâ alikuwa anabofya kinada, huku Mutombo Sozzy akizicharaza drums akisaidiana na Matei Joseph.
Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris âSuper Kongaâ na Pulukulu Wabandoki Motto.Kwa upande wa wanenguaji walikuwa akina âWasha Washaâ, Dulla âPanga Pangaâ, Wandema Rashid, Anna Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima, Zuwena na Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.
Ikiwa katika ukumbi huo wa White House, bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Ngalula, Nasononeka, Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane. Wimbo huo ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.
Zingine zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma, Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo idadi.
Kuna msemo usemao âCha kuazima hakistiri maungoâ msemo huo uliisibu bendi ya Maquis du Zaire baada ya kutokea sintofahamu kati ya mmiliki wa ukumbi na uongozi wa bendi. Hatma yake Maquis du Zaire ikasambaratika, wakaacha ukumbi huo uliokuwa jirani na kona ya kwenda Msewe, ukabadilishwa kuwa gereji hadi leo.
Baadhi ya wanamuziki hao walijikusanya na kuisuka upya bendi hiyo, kwa jina jingine la Maquis Original.Ikaanza kupiga muziki katika kumbi za Wapiwapiâs uliopo Maduka mawili, Changâombe na CCM Kata ya 14 Temeke.
Baadae wakahamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Langâata, Kinondoni walipopafanya kuwa makao yao makuu.
Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Mutombo Lufungula âAudaxâ, Tshimanga Kalala Asossa, Dekula Kahanga âVumbiâ, Mukumbule Lolembo âParashiâ, Mukuna Roy, Ilunga Banza âMchafuâ, Mujos wa Bayeke, Kaumba Kalemba, Mulenga Kalondji âVataâ na wengine wengi.
Maquis Original iliongeza nguvu zaidi kwa kuwaleta wanamuziki wengine toka DRC, muda mfupi kabla ya kuondoka mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga âVumbiâ kwenda Stockholm nchini Sweden.
Wanamuziki hao walikuwa Kivugutu Moto na Chatcho, aliyekuwa akilicharaza gitaa la solo, waimbaji Freditto Butamu na Luhembwe Mwahitwa âBobo Sukariâ.
Safu hiyo ya Maquis Original ilitikisa wapenzi na mashabiki wake katika ukumbi wa Langâata kwa nyimbo zao kali za Mangolibo, Mayanga, Makumbele na nyingine nyingi.Wimbo wa Ngalula ulikuwa ukitia fora mbapo wakati wa âchorusâ, Tshimanga Assosa, alikuwa akimpandisha mori mpiga gita la solo Dekula Kahanga âVumbiâ akimwita âvumbiii⊠Vimbiiii⊠VumbiiiâŠâ
Nyimbo za Maquis Original ziliweza kukonga nyoyo za wapenzi wao kwa mitindo waliyobuni hapo ya âWashawashaâ na âSendemaâ.Aidha Maquis Original walikuwa shabiki wao mkubwa aliyejulikana kwa jina la âMagoma motoâ. Alikuwa akiachiwa uwanja akionesha uhodari wake wa kucheza mtindo hiyo, huku akiwa kajitwisha chupa yenye bia kichwani chake.
Waswahili wanasema kuwa â Lakuvunda halina Ubaniâ Maquis Original nayo ikaondoka katika medani ya muziki, ni zaidi ya miaka 27 sasa toka jina la Maquis Original,liliposambaratika katika miaka ya 1990.
Mwanamuziki mahiri Tshimanaga Kalala Assosa âmtoto mzuriâ, alijitoa Kimasomaso kwa kutumia weledi wake, akalienzi jina la Maquis.
Alianzaisha bendi ya âBana Maquisâ ambayo hupiga na kukumbushia nyimbo zilizopigwa na Maquis du Zaire, Maquis Original na za kwao.Mpenzi msomaji kwa mapenzi yake Mungu, idadi kubwa miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa katika makala hii, wameshatangulia mbele zake.
Wengine wanaumwa maradhi mbalimbali akiwemo Mbombo wa Mbomboka.
Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotangulia mbele zake na awape tahfifu wanaoumwa, amina.
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2CIrch4
via

