Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
WIKI
iliyopita niliendelea kufanya uchambuzi kuhusu maudhui na muktadha wa Ilani za
Uchaguzi za kambi mbili zenye ushawishi katika siasa za mwaka huu; CCM na
Ukawa. Tulianza kutumia vigezo vitatu
kupima ahazi za kila Ilani zinaweza kupimika utekeleza wake au ni ahadi tu za
matumaini!
Vigezo
nilivyotumia ni kama kuitazama ahadi yenyewe iwapo inakidhi hoja ya kuwa suala
linalohitaji kuwekwa katika ilani?Pili tukifungua boksi tutaona ni mkakati gani
ilani inauainisha wa kutekeleza kilichoahidiwa na Je, ilani inaweka kigezo
kinachopimika kwa maana miaka mitano baadaye tukupime vipi kwa lengo lipi?
Tulizichambua
sekta za elimu na maji katika kuangalia Ilani zimeahidi masuala yanayoweza
kupimika? Tulibainisha changamoto katika Ilani hasa ya Ukawa kukosa kuwa na
mkakati wa utekelezaji lakini na vigezo vinavyopimika.
Kwa mfano,
tuliona, katika sekta ya maji Ilani ya Ukawa iliahidi tu: “Tutaweka mazingira rafiki
yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza
kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa
kichwa.”
Tamko
hilo la “mazingira rafiki” halikufafanua sit u mazingira rafiki ni yapi, lakini
lengo ni kuwafikishia maji watanzania wangapi kufikia mwaka 2020 au kuchimba
visima vingapi au kukarabati mabomba au mifumo mingapi.
Hiyo
ilikuwa tofauti kabisa na Ilani ya CCM ambayo kiuchambuzi imetimiza vijenzi
vyetu vitatu vya hoja hapo juu. Kwa mfano inasema: “Kuboresha
huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 53.4 mwaka 2015 hadi asilimia 70 mwaka
2020 kwa kufanya yafuatayo….”
Tulijenga
hojan kuwa ilani hizi mbili katika eneo hili ni milima miwili tofauti kabisa.
Ukawa wanamaanisha kuwa hawana mikakati ya utekelezaji wa wanachoahidi na
watasubiri kuingia Ikulu ndio waanze kuangalia cha kufanya. Unaposema tu
“tutaweka mazingira rafiki ya kila Mtanzania kupata maji safi na salama”
kunaibua maswali.
Mosi ni
mazingira gani hayo “rafiki?” Pili yatawekwa lini na mwisho unaposema “kila
Mtanzania” tunamaanisha nini. Kwamba kufikia mwaka 2020 kila Mtanzania atakuwa
na maji safi na salama?
Leo
tunaendelea kwa kufanya ulinganisho na uchambuzi kama huo kwa kuangalia Ilani
hizo katika sekta za kilimo, nishati na sera za mambo ya nje.
Kilimo
Kilimo ni
sekta nyeti sana nchini. Takwimu bado zinaonesha asilimia zaidi ya 70 ya
Watanzania wanategemea kilimo. Hii haishangazi kuona Ilani zote mbili; CCM na
Ukawa zikiwa na mambo mawili matatu maboresho katika sekta hii.
Ukawa
wanazungumza mambo manne makubwa kuhusu kilimo. Mosi ni kuhakikisha sekta hiyo
inakua kwa asilimia 6-8. Pili, umwagiluiaji. Tatu, maghala ya kuhifadhi mazao
na nne kilimo cha biashara.
Lakini
tatizo langu ni lile lile, ukiacha walivyojitutumua katika ahadi ya kwanza hapo
juu kwa kuonesha namna tutakavyowapima miaka mitano ijayo (ahadi inayopimika ya
kukuza kilimo kwa asilimia 6-8) ahadi zilizobaki ni matamko tu hauonekani
mkakati wala kigezo cha kuwapima.
Hii ni
tofauti na CCM ambao katika ahadi zao za kipaumbele katika sekta ya kilimo kila
moja imewekewa malengo tutakaowapima nao. Mfano, ili kuendelea kuwafikia
wananchi wengi na kuwapa elimu ya kilimo imewekwa lengo la kuajiri maafisa
ugani kufikia 15,082 kutoka 9,558 wa sasa.
Kuhusu
kilimo cha umwagiliaji ilani imefanya uchambuzi na kubaini pamoja na wakulima
wengi kwa sasa kuanza kuhamia katika umwagiliaji badala ya kutegemea mvua pekee
bado lengo ni kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka ekari 461,362 za
sasa hadi ekari 1,000,000 mwaka 2020 na ukurasa wa 12 wameainisha wataitekeleza
vipi ahadi hii.
Hii inampa
mwananchi si tu Imani bali uhakika wa kufuatilia ahadi na kuona utekelezaji
wake. Ilani ya Ukawa hapa tena haikuwatendea haki wananchi inaoahidi kuwaletea
mabadiliko.
Nishati
Sekta ya
nishati ni sekta nyingine muhimu kijamii na kiuchumi na imetendewa haki katika
ilani zote mbili. Ukawa na CCM wote wameweka lengo wanalotaka tuwapime nalo
miaka mitano ijayo la kuongeza/kuzalisha megawati 3,000 (Ukawa) na 4,915 (CCM).
Vyama
vyote vimetaja vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme watakavyovitumia kama
vile gesi asilia, maji na vyanzo vingine mbadala. Tatizo langu na ndio moyo wa
makala hizi ni Je, tunatekeleza vipi ahadi hizi tamu tunazoahidi?
Katika
ilani ya “mabadiliko” ya Ukawa hakuna vijenzi vya hoja yao hiyo. Hakuna ainisho
la mitambo watakayoijenga ya kuzalisha na kusambaza umeme itakuwa wapi na kila
mmoja utazalisha megawati ngapi. Kwa ujumla ilani imemwaga tu ahadi, labda
wakishaingia Ikulu ndio watazinduka!
CCM
wamekuwa “smart” katika hili na kama ilivyo katika maeneo mengi. Kwanza
wameanisha watakavyozizalisha hizo megawati walizoahidi na wanavyoboresha mfumo
wa usambazaji.
Katika
uzalishaji Ilani inaahidi kutekeleza miradi ya umeme iliyoainishwa katika
Mpango Kabambe wa Uzalishaji wa Umeme ambapo kwa ufahamu wangu imo mitambo ya
uzalishaji wa umeme wa gesi minnee Dar es Salaam (ikiwemo Kinyerezi 1 ambayo
iko tayari) na mingine Mtwara na mingine ya vyanzi anuai. Hawa wanamkakati
tayari.
Kuhusu mifumo mipya ya
kusambaza umeme (maana unaweza ukawa na umeme na usiwafikie wananchi), CCM
wametaja kukamilisha miradi mikubwa ya ujenzi wa mifumo mipya ya usambazaji
kama vile Mradi wa Backbone wa kV 400 unaounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga
wenye urefu wa km 670;
Wameainisha Mradi wa
Makambako-Songea wa kV 220, ambao unaunganisha mikoa ya
Iringa, Njombe na Ruvuma
km 250; naMradi wa North-East unaounganisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga,
Kilimanjaro na Arusha. Aidha, mradi mwingine muhimu ni ule wa North-West, ambao
unaunganisha mikoa ya Mbeya, Katavi, Rukwa na Kigoma.
Na kuhusu kusambaza
nishati zaidi ya umeme vijijini, CCM inaanisha mkakati wa kuanzisha REA Awamu
ya Tatu (REA-III) itakayokuwa na lengo pana la kuendeleza kazi nzuri
iliyofanywa sasa lakini pia kuunganisha vijiji zaidi huku mkazo ukiwekwa katika
shule, zahanati na vyanzo vya maji.
Hili ni
eneo jingine ambalo kama kweli mtu anahitaji kuona Ilani ya mabadiliko Ukawa
wamepoteza pointi tatu kabla ya mechi kuanza. Wamezipoteza. Hakuna namna
nyingine zaidi ya kujifunza katika hili.
Mambo ya Nje
Vyama
vyote vimezungumzia Sera ya Mambo ya Nje kwa minajili ya kuendeleza uhusiano wa
kimataifa na kikanda. CCM wamesisitizia kuendeleza sera ya diplomasia ya uchumi
ambayo ni Sera ya Kitaifa.
Ukawa
wameahidi kitu ambacho kimatamko hakipo katika Sera yoyote ya Kitaifa; wanaita
Ushirikiano wa Kimataifa Wenye Tija; sera hii mpya haijafafanuliwa popote kama
inatofauti gani nay a sasa ya Kitaifa.
Lakini
ukisoma ahadi za ndani ya ilani utabaini kuwa wananchoahidi Ukawa kimsingi
hakina kipya zaidi ya kutekeleza matamko yale yale ya sera za sasa ambayo
Tanzania imekuwa ikiyapigania sana kimataifa.
Hata hivyo
moja ya mambo katika uchambuzi wa Ukawa ambayo yanaonesha hawakuwa na mchambuzi
makini katika masuala ya kimataifa ni pale sera yao katika uchambuzi wa “Hali
Halisi” inapoonekana kulaumu kuwa Tanzania ni kama vile imepoteza ushawishi
Kimataifa.
Nikiri,
mimi si mwanadiplomasia wala mwanataaluma katika hili, lakini nipo katika jiji
hili la kitovu cha siasa na diplomasia za Afrika nimestushwa na tamko hilo.
Kwanza tukubaliane kwamba siasa za sasa na jiografia yake (geopolitics) si kama
za miaka 20 iliyopita na wala 40 iliyopita.
Ukisoma
siasa za misimamo za enzi za vita Baridi nitakubaliana nawe kuwa Tanzania nayo
ilipaza sauti yake sana zama hizo. Siasa za sasa kimataifa baada ya mageuzi ya
Urusi na ujio wa sera na ubia mpya wa kiuchumi duniani zina namna yake ya kuzienenda
katika masuala ya kimataifa na kikanda.
Tanzania
katika uwanda huu iko juu sana na inaheshimika dunia na nikiwa nje ya Tanzania
naweza kuthibitisha hili pasi na shaka. Mfano Tanzania licha ya kushika
uenyekiti wa AU na taasisi zake kadha kama vile NEPAD, APRM, Baraza la Usalama
n.k hata UN katika sauti kutoka Afrika zinazosikilizwa sana ni Tanzania.
Tanzania
imeongoza masuala mbalimbali ya kikanda kama vile kushika uenyekiti wa Kamati
ya AU kuhusu Majadiliano na Dunia katika masuala ya tabia nchi. Tumepata
wenyeji kwa maana ya kuwa makao makuu ya Mahakama ya Africa, ICTR, Taasisi ya
Rushwa Afrika (Africa Anti-Corruption Advisory Board) na tumeshika nafasi ya
Naibu Katibu Mkuu wa UN kwa miaka mitano na nusu.
Kama nchi
tumepokea ziara rasmi za Marais na viongozi wote wakubwa duniani kutoka nchi
zote zenye nguvu kama Marais wa Marekani, China, Ujerumani, Katibu Mkuu wa
UNn.k. Diplomasia hii huwezi kuibeza hivi hivi kwa mtu anayefahamu jiopolitiki, sanaa na sayansi za masuala
ya kimataifa.
Kwa hiyo
kiuchambuzi, na nikihitimisha kwa maana ya leo, niseme tu sehemu kubwa ya Ilani
ya Ukawa haijitoshelezi kwa maana ya kuonesha ahadi mbadala, utekelezaji
mbadala wa mambo wanayodhani CCM imekosea kuyafanya.
Badala
yake kama neno mabadiliko linamaa sana ni Ilani ya CCM inayoonesha zaidi ahadi
za mabadiliko si tu kwa minajili ya kuahidi, bali namna Ilani inavyofanya
uchambuzi, inavyokwenda mbele na kuweka mfumo unaoonekana wa kutekeleza na
zaidi kumpa mwananchi uwezo wa kuipima ahadi hizo miaka mitano ijayo kwa kuanisha
malengo yanayopimika ya ahadi.
Ni kwa
minajili hii basi ndio maana anuani ya makala haya inahoji na wiki ijayo
itaendelea kuhoji tena “Tunatoa ahadi zinazopimika au orodha ya matumaini?”
Alamsiki.
*Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania anayefanyakazi katika
moja ya taasisi za kimataifa jijini Addis Ababa, Ethiopia. Kitaaluma ni mtafiti
katika masuala ya siasa na maendeleo.