Katika picha hizo ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia
njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa
Jukwaani huku viungo vyake vya sehemu za siri vikiwa hadharani na zaidi
akionesha tabia ambazo kwa kiasi kikubwa zimefedhehesha na kuidhalilisha
sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla.
Aidha, BASATA limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya
internet kutoka kwa watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la
Msanii huyo. Katika mawasiliano yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na
kudhalilika na tabia hiyo chafu iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe kwamba, Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la
Taifa, hivyo anapokwenda nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua
ya utambulisho kama msanii wa Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi
anatambuliwa kama msanii Mtanzania, anapofanya kinyume na misingi ya
kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe, kazi ya Sanaa na nchi yetu
pia.
Aidha, ikumbukwe kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii
huyu kutokana na tabia yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na
yeye aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo
kuendelea kwake kufanya matukio hayo na kwa sasa katika ardhi ya nchi
nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea
kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na
kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.
BASATA linapenda kueleza kwamba;
Litamuita kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya
onesho hilo la kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii
na Sanaa kwa ujumla
Kama maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa
dhidi yake maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na
hakina uhusiano na kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji
ubunifu, weledi na kujitambua
BASATA linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi
zingine lakini siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka
suala zima la maadili kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya
jamii ya watanzania wanaoipenda na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha.
Tuungane kwa pamoja kukemea kazi chafu zinazozalishwa na wasanii
wasiojitambua kwani suala la maadili ni suala mtambuka na linaanzia
katika ngazi ya familia.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na
taratibu mara wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi.
Linawakumbusha kwamba haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi
dhalili na kuonyesha utupu katika kuvuta mashabiki.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI