RISASI MZIGONI
Mdogomdogo, Risasi Mchanganyiko likajitupa mtaani kuchimba kuhusu madai hayo ambayo awali liliyatilia shaka kama si wasiwasi.
Uchunguzi wetu ulibaini ukweli wa mali za msanii huyo na mambo mengine mengi yanayoingia kama vyanzo vya mapato yake.
MAGARI SITA
Ilibainika kuwa, Masanja anamiliki magari sita, yakiwemo ya kifahari.
Baadhi ya magari hayo ni Toyota Land Cruiser V8, Nissan Hardboad na
Toyota Verossa.
NYUMBA TATU BONGO
Pia,
mkali huyo wa kuvunja mbavu, anamiliki nyumba tatu za maana jijini Dar
es Salaam, moja ni ghorofa ipo Tabata, nyingine Kigamboni na nyingine
haifahamiki eneo rasmi ilipo.
Hata hivyo, imebainika kuwa mbali na mijengo yake hiyo iliyopo jijini Dar, nyumbani kwao Mbarali, Mbeya ana mjengo wa maana.
MASHAMBA KIBAO
Msanii huyo hayupo nyuma kwenye kilimo, ana mashamba kadhaa Kigamboni
jijini Dar es Salaam lakini linalotia fora ni lile lililopo Mbarali
lenye ukubwa wa hekari 50 ambalo analima mpunga.
NI MSANII WAMAIGIZO TAJIRI ZAIDI?
Kwa utajiri huo, ipo minong’ono kuwa, nyota huyo anaweza kuwa kwenye namba za juu za wasanii wa maigizo wenye mkwanja mrefu.
Wengine wanaotajwa kwenye orodha ya waigizaji matajiri Bongo ni Husna
Posh ‘Dotnata’, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ na Amri Athumani ‘Mzee
Majuto’.MATAJIRI BONGO FLEVA
Katika muziki wa Bongo Fleva, wasanii wanaoaminika wana utajiri mkubwa
zaidi ni Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Joseph
Haule ‘Profesa Jay’.
Wasanii hao wanamiliki mijengo ya maana, achilia mbali magari ya kifahari na miradi kadhaa.
MASWALI KUHUSU MASANJA
Utajiri wa Masanja umeonekana kuibuka ghafla huku vyanzo vyake vya
kumwingizia kipato vikijulikana ni sanaa ya uigizaji, muziki na huduma
ya uchungaji.
Je, kwa uigizaji tu katika Kundi la Orijino Komedi ‘OK’ ndiko alikopata mkwanja huo na kuanzisha miradi hiyo mikubwa?
Kama ndiyo, kwa nini memba wenzake ndani ya kundi hilo hawana maendeleo makubwa kama yeye?
Kazi nyingine ya Masanja ni muziki wa Injili ambapo kwa sasa albamu
yake ya Hakuna Jipya iko sokoni. Je, albamu hiyo na shoo anazofanya
zinaweza kuwa chanzo cha utajiri huo?
Lakini pia Masanja ni mchungaji ambaye anahudumu katika Kanisa la
Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) ‘Mito ya Baraka’ lilicho
chini ya Askofu Bruno Mwakiborwa. Je, mshahara anaoupata kutokana na
huduma hiyo unaweza kuwa chanzo cha mapato yake?
Risasi Mchanganyiko halikutaka kupasua kichwa, juzi lilimsaka Masanja
kwa simu na kumhoji juu ya mali zake ambapo kwanza alithibitisha kweli
anamiliki mali hizo na nyingine ambazo hakupenda kuzitaja.
“Ni kweli nina nyumba tatu hapa mjini, kampuni ya ulinzi na mashamba
ya mpunga eka 50 nyumbani Mbarali, Mbeya. Kuhusu magari pia ni kweli
kabisa. Mimi ni mtumishi sitakiwi kusema uongo,” alisema Masanja.
RISASI: Lakini mbona utajiri wako umekuwa wa haraka sana mtumishi, vipi vyanzo vya mapato yako?
MASANJA: Orijino Komedi ndiyo chanzo cha vyote… pale ndipo kwenye koki.
RISASI: Kuchekesha tu kaka? Au kwenye muziki wa Injili pia kunalipa?
MASANJA: Injili na uchungaji ninaotumika kanisani ni huduma kaka,
sitegemei mapato kutoka huko. Nipo kwa ajili ya kulisha kondoo wa Bwana.
RISASI: Wasanii wenzako wa Orijino Komedi wanachukuaje mafanikio yako?
MASANJA: Wanafurahia, wananiunga mkono maana ni sehemu ya mafanikio yao
pia. Sisi tunaishi kama ndugu. Kwa hiyo kuna baadhi ya aidia ni zao,
hivyo wanajivunia sana mafanikio yangu.
Tuituitui! Simu ikakatika! Risasi likaenda mtamboni.
CHANZO:RISASI MCHANGANYIKO