SWALI KWA WAGOMBEA URAIS WOTE UMELISOMA??….JE?WANASIASA WETU MNATOA AHADI ZINAZOPIMIKA AU ORODHA YA MATUMAINI?-3

Admin Updates9 years ago6 Views

Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
MAKALA iliyopita katika mfululizo wa Makala hizi kuhusu Ilani za vyama katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 niliangalia sekta za kilimo, nishati na mahusiano ya kimataifa. Tuliona tofauti kati ya vyama vinavyotoa ahadi zinazopimika na vile vyenye orodha ya matumaini.
Makala ya leo, nitahitimisha kuhusu uchambuzi wa Ilani za vyama hivi vikuu viwili CCM na Chadema/Ukawa kwa kuiangalia sekta muhimu ya miundombinu. Katika kudadisi, swali letu ni lile lile la kidadisi: Je, tukitazama Ilani hizi kwa macho matatu, katika sekta muhimu kama ya miundombinu, kuna ahadi zinazoweza kupimika na kuwa tumaini la kweli kwa wananchi au ni mwendelezo wa ahadi ninazoweza kuziita za mageresho. Tuangalie reli, Bandari na barabara.
Reli
Hakuna ubishi kwamba usafiri wa reli ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi na wananchi wake. Ilani zina maono gani kuhusu reli? Katika hili ilani zote zimejaribu kuainisha mkakati wao katika nyanja hii ya uchukuzi.
Lakini cha kushangaza, ama ikiwa ni kukosa muda wa kutafiti au kupanga mambo yao vyema, Ukawa katika Ilani yao kuhusu reli wamefanya mambo mawili tu; mosi, ni kulalamika na pili kuahidi ahadi isiyo na matumaini.
Ilani ya Ukawa inalalamika kuwa Serikali ya CCM imetelekeza reli, jambo ambalo kwanza si kweli kwa sababu ukweli ni kwamba kuna maboresho makubwa yamefanyika lakini hata kama ingekuwa hakuna maboresho kabisa yaliyofanyika swali ni Je, washika bendera wa Ukawa ambao ni Lowassa na Sumaye waliokaa madarakani kipindi kirefu walifanyanini?
Na bahati mbaya kwamba hata baada ya kulalamika huko, badala ya kuweka mkakati unaopimika wa kuboresha usafiri wa Reli Ukawa kama kawaida yao wanasema tu: “Kujenga reli mpya na kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa kwa kuzingatia maslahi ya nchi . Hii ni pamoja na kujenga uwezo wa kuzalisha mataluma ya reli nchini.”
Wakati Ilani ya Ukawa ikiishia kulalamika tu, CCM wamekuwa “smart” zaidi kwa kwanza kuainisha wamefanya nini katika kuboresha usafiri wa reli na taasisi zinazosimamia reli (Ukawa hawakugusa kabisa suala la taasisi za usimamizi wa sekta ya reli. Haliwahusu!).
Lakini Ilani ya CCM imezungumzia shirika la reli ikisema: “Shirika la Reli nchini (TRL) limeendelea kuimarishwa kwa kufanya yafuatayo:-Kununua na kukarabati vifaa mbalimbali (vichwa vya treni, mataruma, na mitambo ya kunyanyulia mabehewa).
“Kutandika reli za ratili 80 kwa yadi kutoka Kitaraka hadi Malongwe (kilometa 89);  Ujenzi wa Madaraja makubwa matatu ya stesheni za Kilosa na Gulwe; na stesheni za Bahi na Kintinku; na (ii) Kwa upande wa shirika la TAZARA, vichwa vya treni vya njia kuu vipya sita (6); mabehewa ya mizigo 90; vipuri vya matengenezo ya vichwa vya treni vitatu (3); na ukarabati wa mitambo ya kunyanyulia mizigo vinne (4) vimenunuliwa na ukarabati umefanyika.”
Na wakati pia Ukawa wakilalamika tu, CCM wao katika Ilani wanakwenda mbele zaidi kwa kutaja nini hasa kimefanyika katika upanuzi au ujenzi wa reli inaposema: “Aidha, mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na Zambia yanaendelea ili kuboresha shirika hilo.”
“(b) Ujenzi wa Reli Mpya Upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Reli mpya ya Dar es Salaam-Kigali (Rwanda) na Msongati (Burundi) kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) umekamilika. Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa kutoka Isaka hadi Mwanza umekamilika.”
Hapa kimsingi ni sawa na kusema Ukawa wanapagawa kwa kutumia Ilani kulaumu tu, CCM inatekeleza na kuwaomba wananchi waungane nayo kuendeleza mageuzi. Ukawa wanasubiri wakiingia Ikulu ndio waanze kuhaha ni reli zipi za kuzifanyiakazi na waanzie wapi, CCM wameanisha wamefanya nini, watafanya nini na kwa malengo na mkakati upi?
Bandari
Kama ilivyo katika sekta nyingine hata Bandari pia Ukawa hawakuona hoja wala haja ya kuwa na mkakati unaoonekana. Tamko kama: “Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya,” hakujitoshelezi, kuna kupwaya kwa wazi na ni aibu kwa Ilani inayodai ni ya mabadiliko!
Wakati Ukawa wakichachawa hivyo ilani ya CCM imeainisha kwa kina maboresho yanayoendelea katika kuboresha Bandari zote ikiwemo za kwenye maziwa. Imetaja bayana kwamba maboresho haya yataendelezwa na nini kitafanyika katika kila Bandari.
Barabara
Kama kuna eneo jingine ambalo Ilani ya Ukawa imeendeleza mageresho badala ya ahadi tunazoweza kuwapima miaka mitano ijayo ni hili. Ilani inayojinasibu kuleta mabadiliko inapoishia tu kusema: “Kujenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora hasa zile za vijijini,” (uk wa 40 wa Ilani) haiwezi kumuaminisha mtu kuhusu mageuzi yanayoimbwa.
Badala yake Ilani ya CCM imejipambanua kuwa yenye kuleta mageuzi halisi na ambayo wananchi watakuwa na nafasi ya kuona na kuhoji utendaji wake miaka mitano ijayo. Ni Ilani pekee iliyoweka malengo yanayoonekana na kupimika na kutekelezeka.
CCM, tuwape kongole lao, katika hili wamejionesha kweli wamedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli. Katika uwanda wa barabara Ilani iko wazi. Imefanya tathmini barabara zinazohitajika nchini ni ngapi, ngapi zimejengwa kwa lami, ngapi bado na ikaweka mkakati madhubuti wa utekelezaji wa ujenzi.
Ukisoma ukurasa wa 40 wa Ilani ya CCM utaona orodha ya barabara zote ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Kisha inafuatia orodha ya barabara zote ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Zimeainishwa bayana.
Ilani ya CCM inakwenda mbele zaidi kwa kuorodhesha barabara ambazo zimefanyiwa upembuzi yakinifu na ujenzi kuwa umeanza kwa kiwango cha lami katika baadhi ya maeneo (uk wa 42).
Ilani inaongeza kwa kuainisha vyanzo vya fedha zitakazotumika kuendeleza ujenzi wa barabara nchini. Kunatajwa pia Mfuko wa Barabara (Road Fund) ambao utapewa fedha kutoka vyanzo mbalimbali
Mkakati mwingine wa utekelezaji uinaainishwa kuwa ule wa kufikiria kuanzisha taasisi/wakala maalum atakayeshughulikia ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na katika ngazi ya Halmashauri.
La mwisho kwa maana ya barabara, tofauti na Ilani ya Ukawa iliyoahidi tu kwa sentensi moja, Ilani ya CCM imekwenda mbali kwa kiwango cha kuweka malengo ambayo kwayo wananchi watayapima katika miaka mitano ijayo-haya ni mabadiliko ya hakika.
Kwa mfano, wakati ile ya Ukawa ikiwa kimya, Ilani ya CCM inaweka lengo la kuanzisha ujenzi mpya au kukarabati kilometa 5,427 za barabara na zimetajwa (uk. 48). Ipo pia ahadi ya kujenga kilometa 1055 za barabara kuu na za kimkakati na zimetajwa (uk 49).
Ni kwa minajili hii basi bado ni wasilisho langu kuwa ahadi za mabadiliko kimsingi ni ngumu kuziona katika Ilani ya Ukawa badala yake mabadiliko hayo ya msingi unayaona sawia kabisa katika Ilani ya CCM.
Sisemi kwamba Ilani ya Ukawa imeshindwa kuakisi mabadiliko wanayoyaimba kwa sababu tu namna ilivyoshindwa kwa kiwango kikubwa kuwa na ahadi zinazopimika, yako mengi zaidi yanayoifanya Ilani hiyo kuwa na udhaifu mkubwa usioakisi mabadiliko wanayoyaimba.
Wiki ijayo tutatumia muda kidogo kuangalia kwa kina kasoro/madhaifu 10 katika Ilani ya Ukawa yanayoifanya Ilani hiyo kukosa uhalisia wa kile inachojinasibu nacho; mabadiliko.
Alamsiki.

*Mwandishi wa makala haya ni Mtanzania anayefanyakazi katika moja ya taasisi za kimataifa jijini Addis Ababa, Ethiopia. Kitaaluma ni mtafiti katika masuala ya siasa na maendeleo.
Join Us
  • Facebook38.5K
  • X Network32.1K
  • linkedin12.6k
  • youtube23.4k
  • Instagram18.9K

Stay Informed With the Latest & Most Important News

I consent to receive newsletter via email. For further information, please review our Privacy Policy

Categories
Loading Next Post...
Follow
Sign In/Sign Up Search Trending 0 Cart
Popular Now
Loading

Signing-in 3 seconds...

Signing-up 3 seconds...

Cart
Cart updating

ShopYour cart is currently is empty. You could visit our shop and start shopping.