Na: Moshy Kiyungi,Tabora.
Kundi la wanamuziki wa bendi ya Zaiko Langa Langa, walimuacha kiongozi wao Nyoka Longo, wakutokomea wakiwa nchini Marekani.
Kwa mujibu wa habari zilizotangazwa na mwanamuziki nguli Tshimanga Kalala Assosa, kupitia redio moja humu nchini hivi karibuni, alisema wanamuziki hao walikuwa katika ziara ya kikazi katika mji wa Los Angles nchini humo.
Walikuwa katika maonesho kadhaa, baada ya onesho lao la mwisho, wanamuziki wote walitoweka kusikojulikana huku wakimuacha kiongozi wao Nyoka Longo, asijiue la kufanya.
Zaiko Langa Langa ni bendi iliyojizolea sifa tangu na bado inaendeleza umaarufu wao tangu kuanzishwa kwake miaka ya sabini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bendi hiyo ‘imewapaisha’ wanamuziki wengi ambao nao walijipatia umaarufu mkubwa wakiwamo akina Papa Wemba, Bozi Boziana, Dindo Yogo, Evolocko Jocker na Nyoka Longo wote ni kizazi cha Zaiko Langalanga.
Kama ilivyo Wenge Musica na makundi yake, Zaiko nayo imefanikiwa kuzaa bendi nyingi kama Isifi Lokole, Viva La Musica, Langa Langa Stars, Zaiko Familia Dei, Anti Choc, Choc stars, and Zaiko Nkolo Mboka.
Zaiko Langa Langa ilianzishwa rasmi mwaka 1970 wakati huo ikijulikana kama Orchester Zaiko, waanzilishi wakiwa ni Papa Wemba, Evolocko Lay Lay, Zamungana na Nyoka Longo.
Baadaye washabiki wakaanza kuwaita Langa Langa wakimaanisha ‘kulewa’ kwa kuwa nyimbo zao zilikuwa zikipigwa sana kwenye vilabu vya pombe kila kona.
Zaiko ndio waanzilishi wa sebene la leo ambapo wao walichukua mtindo wa kiasili na kuingiza ala kama magitaa, Chants, na rap kwa mbali jambo lililonogesha muziki wao na kuufanya kupendwa na rika lote.
Mwaka 1973 Zaiko walikuwa maarufu sana si tu kwa Zaire bali hata kwa nchi za jirani huku mwanamuziki wake Evolocko Jocker akiwa ni maarufu sana kwenye bendi hiyo ambapo aliweza kuingiza mtindo maarufu wa cavacha wa uchezaji ambao ulikuwa maarufu sana na kupendwa kote.
Miaka ya kati kati mwa sabini bendi hii ilianza kumong’onyoka ambapo waliondoka walikuwa wanamuziki wake maarufu kama Papa Wemba.
Wengine ni Bozi Boziana, Evolocko na Mavuela ambao kwa pamoja walianzisha Bendi iliyoitwa Isifi Lokole, ambayo hata hivyo haikukaa sana kwani nayo ilimeguka na kutoa bendi mbili Yoka Lokole, na Viva La Musica ya Papa Wemba.
Mwishoni mwa miaka ya sabini Bendi ilikuwa iko juu si mchezo huku wanamuziki wake wakiwa wanasifika kwa kila kitu, inakumbukwa wanamuziki kama Nyoka Longo, Lengi Lenga, Bimi Ombale, Dindo Yogo, Evolocko walileta laha sana kwenye bendi hii.
Ilienda mpaka miaka ya mwanzoni mwa 80 ambapo bendi ilimeguka tena. Hii ilitokana na wakongwe kama Meridjo, Nyoka Longo na Dindo Yogo kutokubaliana na mambo waliyoyaita mageuzi ambayo yaliletwa na vijana wapya kama Lengi Lenga, Ilo Pablo na Bimi Ombale.
Hii ilipelekea kusambaratika na kundi la akina Nyoka Longo likajiita Zaiko Langa Langa Nkolo Mboka, na lile la Bimi likajiita Zaiko Langa Langa Familia Dei.
Makundi yote kwa pamoja na mafanikio na mchango mkubwa kwenye ulimwengu wa muziki wa Kongo.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0767331200, 0736331200, 0784331200 na 0713331200.
from MICHUZI BLOG https://ift.tt/2SiwYN0
via