
KIGAILA: Mbowe Hakutaka Chadema Igawanyike Kabisa, Lissu Alianza Kutugawa Baada ya Kushinda
“Sisi tumeamua wote kwa pamoja tunajiondoa Chadema ili tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka kwasababu sisi hatuwezi kuwa sehemu, hatuwezi kuwa wanachama wa Chama ambacho maamuzi yake hayafanywi kwa vikao, hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambacho wanachama wanabaguliwa, hatuwezi kuwa wanachama wa chama ambacho Katiba haifuatwi. Hatuwezi kuwa wanachama wa namna hiyo kwasababu sisi sio chawa, sisi ni Viongozi, sisi tunajitambua na tuliingia Chadema kwasababu ya malengo na tunatoka Chadema kwasababu Chadema imeachana na malengo yaliyotufanya tuingie.
Kwahiyo tunajitoa Chadema ili wasipate sababu kwamba Chama hiki kilikufa kwasababu walikuwepo. Na ili nisiwaachie maswali mtu anaweza akauliza sasa tunaenda wapi, sisi sio wazee wa kufikia umri wa kustaafu. Tutaendelea kuwapigania watanzania na tutatafuta jukwaa muafaka.”
“Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe baada ya kushindwa uenyekiti alizungumza mambo kadhaa, jambo la msingi kuliko yote alitoa ushauri kwenye chama kuvunja makundi, kukiunganisha chama, na kuunda Tume au Kamati ya Maridhiano ili chama kiweze kurudi pamoja, kiweze kurejea kwenye kazi yake ya kupigania haki, uhuru na maendeleo ya watu, kwahiyo aliweka bayana namna hiyo. Lakini sisi tuliokuwapo, tuliokuwa tunasikiliza na kuangalia tulishtushwa na kitu kimoja! Mwenyekiti aliyekuwa ameshinda na kutangazwa, wakati anaongea baada ya Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kuongea, aliendelea kumshambulia mgombea mwenzake kana kwamba kampeni zinaendelea. Na kwa maana hiyo, shambulio la Mwenyekiti aliyekuwa amechaguliwa, Mheshimiwa Tundu Lissu dhidi ya Mwenyekiti aliyekuwa anamaliza muda wake Mheshimiwa Freeman Mbowe, mbele ya wajumbe baada ya uchaguzi ilipeleka ujumbe kwa wafuasi wake kwamba kampeni bado zinaendelea. Kwa hiyo, ambacho kinaendelea kwenye chama kuanzia siku ile mpaka leo, ni ubaguzi mkubwa wa wanachama ambao wanaitwa ni timu ya Mbowe, wanabaguliwa kuanzia kwenye kamati kuu mpaka kwenye misingi”, – Kigaila.
Benson Kigaila, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bara akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika kati ya waliokuwa Wajumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA taifa mpaka tarehe 22 Januari 2025, na wanahabari mkoani Dar es Salaam siku ya Jumatano.
Benson Kigaila, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bara akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika kati ya waliokuwa Wajumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA taifa mpaka tarehe 22 Januari 2025, na wanahabari mkoani Dar es Salaam siku ya Jumatano.